Na. Faraja Mbise, DODOMA
Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kuwajengea uwezo wa kimbinu na kuwatumia wataalam wa ndani ili kuongeza mapato ya ndani sambamba na kubuni miradi ya kimkakati yenye tija kwa maendeleo ya nchi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, waliotembelea Dodoma kwa lengo la kujifunza na kuongeza wigo wa namna sahihi ya kuongeza mapato ya ndani kupitia miradi mbalimbali, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Hakuna mapato madogo na hakuna mradi mdogo, ila tunapoandaa miradi, tujiulize tunaandaa miradi yenye mfumo gani?. Kwahiyo, tunavyofikiri miradi, hata yenye mtazamo wa kibiashara lazima tufikirie kwenye kukua kwake. Hivyo, kila kitu kinaweza kikaanza kwenye udogo, kikakua na mapato yaleyale madogo tunaweza tukaanzisha miradi kwa mapato ya ndani. Nilichokuwa nataka kusema cha kwanza ni kutumia wataalam ili kutuongoza katika namna bora ya kutekeleza miradi hiyo” alisema Dkt. Sagamiko.
Akizungumza kuhusu ziara ya Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, aliwataka watumie fursa hiyo ya ziara ili kuongeza nguvu katika kutekeleza miradi. “Naomba ziara hii itumike kuwajenga, kuwaongezea nguvu zaidi, kwamba tulipo tunaweza kufanya pakubwa zaidi badala ya kuwakatisha tamaa, ni kweli tumekuja kujifunza miradi. Lakini kikubwa tumekuja kutanua fikra zetu, tupate matamanio ya mambo ya kwenda kufanya Kyerwa, kikubwa tumekuja kupanua wigo” alisisitiza Dkt. Sagamiko kwa kauli ya kutia moyo.
Aidha, aliwataka watumishi wa serikali kukubaliana na maeneo ambayo wamepangiwa kazi, hata kama yana miundombinu mibovu wasihame na kuwataka wao ndio wawe chachu ya maendeleo ya sehemu hiyo na kutokimbilia mijini.
“Watumishi tuna ‘tendency’ ya kwenda mahali ambapo ni pazuri, lakini hatujui kwamba kuna watu walifanya kazi mahali pale kuwa pazuri. Dodoma ilikuwa kama Kyerwa, lakini kuna watu wakafanya kazi, hakuna sehemu yoyote kabla ya uhuru tukasema ilikuwa kama vile ilivyo, hata Kyerwa hayo maendeleo mnayoanza kuyaona, kasi imeongezeka baada ya kuwa wilaya. Sisi binadamu wengi tunakuwa wavivu wa kufikiri, wengi tunatamani kwenda kutumia vya wenzetu kuliko kutengeneza vile tunavyotamani sisi.
Tunaona tunakuja kupata changamoto, watumishi hawashiriki kufanya ‘transformation’ ya maendeleo ili waweze kuyaweka matamanio ya sehemu wanayoishi” alisema Dkt. Sagamiko.
Sambamba na hayo, aliwaasa kusimamia miradi ambayo wanaianzisha ili iwe na matokeo chanya, kutumia mapato ya ndani kwa busara na kufanya uwekezaji popote pale nchini pasi na kuwa na mipaka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, kutoka Mkoa wa Kagera, SACF. James John, aliipongeza Hamashauri ya Jiji la Dodoma kwa uthubutu wa kufanya mambo makubwa zaidi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Sanjari na hayo, alieleza sababu ya kuelekeza ziara yao katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Tumetembelea miradi kadha wa kadha, ambayo imejengwa katika namna tatu. Kwanza, mapato ya ndani, pili, fedha kutoka serikali kuu na tatu, kutoka ufadhili wa Benki Kuu ya Dunia.
Kimsingi miradi yote imenivutia kwasababu inaonesha tija na hadhi, kilichonivutia zaidi ni mradi wa Shule ya Dodoma English Medium School, kwasababu inatumia mtaala wa lugha ya kingereza kufundishia.
http://WATAALAM WATUMIKE KUKUZA MAPATO YA NDANI.Kwanini, tumekuja Dodoma, ni kwasababu ya kuwaonesha madiwani uthubutu waliokuwa nao wenzetu katika Jiji la Dodoma. Jiji la Dodoma sio kuwa linapata mapato makubwa zaidi nchini Tanzania, lakini wamefanya mambo makubwa zaidi kuliko halmashauri nyingi, tulichokiona zaidi ni uamuzi na uthubutu wa wataalam na madiwani katika kutekeleza miradi ya maendeleo” alisema SACF. John.
Akiongelea mambo ambayo amejifunza katika ziara hiyo, Diwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Devota Biashara, alisema “katika miradi yote tuliyozunguka, nimevutiwa haswa na mradi wa shule, katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kyerwa nasi tunampango wa kujenga shule itakayotumia mtaala wa kingereza kufundishia. Kwahiyo, nilipoona mradi huu unaendelea vizuri na tulipoolezwa, hakika nilifurahi na nilijifunza vitu vingi. Jambo lingine, nimejifunza uthubutu, tukitaka kuamua kitu tunakuwa waoga, lakini ziara hii imetujengea ujasiri”