Akikabidhi vifaa hivyo, Mheshimiwa Nnauye amewataka wazazi na walezi kuwalinda watoto dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ikiwa ni pamoja na kuwambia ukweli juu ya faida na hasara za matumizi ya TEHAMA ili kujenga kizazi ambacho hakijaharibiwa na kasi ya ukuaji wa maendeleo ya kiteknolojia.
“Ni matumaini yetu vifaa hivi vitatumika kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma za elimu katika shule yetu, ninaamini kuwa ufaulu utaongezeka na uwezo wenu wa kukabili mazingira pia utaongezeka” aliongeza Waziri Nnauye.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mheshimiwa Anthony Mavunde amemshukuru Waziri Nnauye kupitia UCSAF, kwa kuhakikisha kuwa shule hiyo inapata vifaa vya TEHAMA ili kusaidia katika kuboresha kiwango cha elimu shuleni hapo.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF John Munkondya amesema, UCSAF imetoa komputa tano kwa shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa mradi wa kuzipatia shule za umma vifaa vya TEHAMA na kuziangusha na mtandao wa intaneti.
Kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 UCSAF imetoa vifaa hivyo kwa shule 811 za Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo kila shule ilipata wastani wa komputa tano na printa moja.
Pia ameahidi kuwa taasisi hiyo itahakikisha kuwa walimu katika shule ya Sekondari Chinangali wanapatiwa mafunzo ya matumizi bora ya vifaa hivyo ili viweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
“Baada ya kukabidhi vifaa hivi tunaomba walimu wataochaguliwa waingie katika mpango wa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu kwa mwaka wa Fedha 2022/2023”.
Akitoa shukrani kwa niaba ya shule, Afisa Elimu Sekondari Bi. Upendo Rweyemamu ameipongeza UCSAF kwa kutekeleza mradi huo huku akitoa wito wa kuendelea kuzifikia shule nyingine za sekondari zilizoko katika Mkoa wa Dodoma.