Na; Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM
Chemba ya wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC) imeishukiru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali na kuwawezesha kuuza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam, na Mwenyekiti wa TWCC Taifa, CPA Mercy Silla, katika hafla ya kutambua bidhaa za wanachama wao zilizopata cheti cha ubora wa viwango kutoka Shirika la Viwango Tanzania – TBS.
CPA Silla amesema TWCC kwa kushirikiana na Idara mbalimbali za Serikali kumekuwa na jitiada kubwa za kuhakikisha changamoto za wajasiriamali nchini zinafanyiwa kazi, sambamba na kutoa mafunzo ya namna bora ya kufanya biashara na kuwawezesha kuyafikia masoko makubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
‘TWCC tunaendelea kuwahamasisha na kuwaunga mkono wanachama wetu waweze kuona ni jinsi gani tunavyoweza kwenda nao, kuwakuza pamoja na kusikiliza hoja na maoni yao juu ya changamoto mbalimbli wanazopata kwenye biashara ili kuzipatia ufumbuzi na kuendelea kufanya biashara zao’ amesema CPA Silla
Amesema katika kulifanikisha hilo wamekuwa wakiendesha mafunzo ya ndani na nje kwa kuwapeleka wajasiriamali wao nchini China ili kuwajengea uwezo zaidi na kujifunza mbinu mbalimbali za kibiashara.
Kwa upande wake mjasiriamali anayezalisha bidhaa za sabuni ambazo zimepata nembo ya ubora wa TBS, Magreth Lifa Kyejo, amesema pamoja na hatua kubwa waliyopiga kwa bidhaa zao kupata cheti cha viwango, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa malighafi na vifungashio, hivyo kuiomba Serikali kuzishughulikia ili kuwapunguzia gharama za uzalishaji.
‘Sisi kama wajasiriamali tunapata tabu kwenye malighafi na vifungashio, tunaleta kilio chetu kwa Serikali ili waliangalie hili na kutusaidia kwani tunashindwa kumudu gharama za uzalishaji, tunaomba ikiwezekana kuwepo bei maalum kwaajili ya wajasiriamali peke yao’ amesma Bi Kyejo.
Naye, Mwenyekiti wa GSM Enterprises Limited Bw. Sais Kyejo amesema wajasiriamali wengi wamekua wakifanya vizuri katika kuzalisha bidhaa zenye ubora lakini wanakabiliwa na changamoto ya mitaji, ambapo ameiomba Serikali kuimarisha suala la mikopo ili kuwepo na wajasiriamali wengi watakao zalisha bidhaa zenye ubora na kuongeza wigo wa biashara kwa kuuza bidhaa zao mahali popote Duniani.
TAZAMA VIDEO