Rais Samia Apongezwa Kuifungua Nchi Kiuchumi
Dkt. Biteko Awahimiza Wafanyabiashara Kulipa Kodi Kwa Maendeleo ya Nchi
TCCIA Yaendelea Kuwa Daraja la Wafanyabiashara wa Tanzania, Yafungua Ofisi China, London na Uturuki
Serikali Yapongezwa Kwa Kuwekeza Kwenye Miundombinu
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Serikali imesema itaendeleza jitihada zake za kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara kwa lengo la kuboresha shughuli za biashara, uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
Sambamba na kushirikiana na sekta binafsi ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini ikiwa ni pamoja kujenga na kuimarisha miundombinu kwa ajili ya usafiri na usafirishaji.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Desemba 6, 2024 jijini Dar es salaam wakati akifungua Kongamano la Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi Mwaka 2024 na Mkutano Mkuu wa 49 wa Mwaka 2024 wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).
Dkt. Biteko ameeleza umuhimu wa sekta binafsi na kusema kuwa nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla inakisiwa kuwa vijana wengi ambao wanaingia katika soko la ajira wanategemea sekta binafsi ndio maana Serikali imeendelea kushirikiana na kutatua changamoto za sekta binafsi.
“ Hivi karibuni mlitoa malalamiko kadhaa ikiwemo ya kukwamisha shughuli za biashara na Serikali imeyatatua kwa kushirikiana nanyi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja baadhi ya jitihada zilizofanywa na Serikali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kuwa ni pamoja na kufanywa marekebisho ya sheria na kanuni 55 na sheria zingine 16 na kanuni zake zinaendelea kufanyiwa kazi.
Amesisitiza “ Serikali imeondoa mwingiliano wa majukumu na kuanzisha mamlaka mfano sasa tuna Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kurahisisha shughuli zenu. Pia, imepunguza idadi ya muda wa kupata huduma kutoka siku 14 hadi tatu na kutoka siku saba hadi tatu za kusafirisha mizigo kutoka Dar es salaam hadi Tunduma.”
Pamoja na hayo Dkt. Biteko amefafanua kuwa Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA) imepunguza tozo 16 za biashara ambazo kupitia hizo Serikali inapoteza mapato kiasi cha shilingi bilioni 37 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi na jitihada za Rais Samia za kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Fauka ya hayo, amezungumzia viashiria vya ukuaji wa uchumi na kusema kuwa kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme ambapo awali hayakuwahi kuzidi megawati 219 kwa mwaka na kuwa mwaka 2024 mahitaji ni megawati 420.
“ Mkifanyabiashara maana yake mahitaji ya nishati ya umeme yanaongezeka na hii ni kwa sababu viwanda vingi vimejengwa na uchumi unachangamka. Tunaanza kuona wananchi wanatumia umeme megawati 52 na viwanda vinatumia megawati 48 hii ni kiashiria kuwa uchumi unaendelea kukua vizuri,” amebainisha Dkt. Biteko.
Vilevile, amewaasa wafanyabiashara nchini kulipa kodi kwa hiari ili Serikali iweze kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali itakayosaidia utoaji huduma za kijamii kwa wananchi na kuchochea maendeleo huku akiwataka kuzalisha malighafi na bidhaa zenye ubora zitakazovutia masoko na kutoa ajira kwa watu.
“Nchi yetu tutaijenga wenyewe na tuambiane ukweli kwamba kulipa kodi ni wajibu wetu, kwa mikataba hii iliyowekwa saini hapa leo TCCIA muwe mawakala wa kutoa elimu ya mlipa kodi kwa wananchi ili watu waone heshima ya kulipa kodi,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini huku akivitaka vyama vya kisekta kuepuka migogoro na kusisitiza upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. John Lukuvi amesema kusanyiko hilo la zaidi ya wafanyabiashara na wakulima 300 kutoka nchi nzima ni muhimu na kuwa kupitia jukwaa hilo Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kukuza sekta binafsi nchini.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo amesema kuwa Mkoa huo umekuwa na ushirikiano mzuri na TCCIA katika shughuli mbalimbali.
“Wafanyabiashara hawa wamekuwa wakipongeza jitihada za Rais Samia kwa kupunguza msongamano wa meli bandarini, kuboreshwa kwa miundombinu wezeshi ya viwanda mfano zaidi ya shilingi trilioni moja imetolewa katika miradi ya barabara ya DMDP na sasa umeme uko wa kutosha na wanaendelea kufanya biashara vizuri,” amesema Mpogolo.
Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Vicent Minja kwa niaba ya wafanyabiashara nchini amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuifungua nchi na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania na hivyo kusaidia biashara kufanyika kwa utulivu.
Amesema taasisi yake ina ofisi katika nchi za China, Uturuki na Uingereza na hivyo inarahisisha kuunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na nchi mbalimbali.
“Tunaishukuru Serikali kwa kurahisisha maendeleo ya biashara katika Bandari ya Dar es salaam sasa meli zikija na mizigo zinapakuwa ndani ya siku chache, pia tunamshuru Rais Samia kwa kuunda tume ya kushughulikia masuala ya kodi,” amesema Minja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kissanga amesema kuwa taasisi yake inalenga kuunganisha wadau wa biashara na kukuza sekta ya biashara na kilimo nchini.
“Katika kipindi cha miaka 36 TCCIA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha ushindani na kuvutia wadau wa ndani na nje ya nchi,” amesema Kissanga
Ameongeza kuwa lengo TCCIA ni kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo endeleo na kujenga uchumi imara huku akimpongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuhakikisha kunakuwepo na ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi.
Kissanga ametaja baadhi ya utekelezaji wa shughuli za TCCIA katika kipindi cha mwaka 2024 kuwa kutoa mafunzo ya kuelimisha Watanzania kuhusu Soko Huru la Afrika kutoka katika mikoa nane, imesafirisha shehena za bidhaa mbalimbali katani ikiwa ni asilimia 70 ya shehena yote.
Vilevile, imefanya ukaguzi wa viwanda 37, na kufanya Jukwaa la Biashara ya Korosho Tanzania na kuleta nchini zaidi ya kampuni 100. Sambamba na kuzisaidia kampuni za Tanzania kupata fursa za uwekezaji na masoko kutoka nchi mbalimbali duniani.
Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Trademark Afrika, Elibariki Shammy amesema taasisi yake inalenga kuisaidia Watanzania na Afrika kwa ujumla ili iweze kufanyabiashara na dunia na kuwa ina wadau kutoka sekta ya umma na binafsi na hivyo wanashukuru kwa kuendelea kuaminiwa katika kutekeleza shughuli zao.
Aidha, kupitia Kongamano hilo Dkt. Biteko ameshuhudia utiaji saini wa baadhi ya mkataba ikiwemo mkataba kuwezesha kufanya kazi pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, ushirikiano wa biashara kati ya TCCIA na Chuo Cha Biashara (CBE) ambapo CBE inatarajia kuwa na mitaala ya biashara ya wanagenzi na hivyo ushirikiano huo utasaidia kufikia wafanyabiashara watakaosaidia kufundisha wanafunzi.
Mkataba mwingine uliowekwa saini ni wa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wanachama wa TCCIA kulipa kodi kwa hiari kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kurahisisha ulipaji kodi na kutoa elimu ya namna kiwango na muda wa kulipa kodi.
Kongamano hilo limeongozwa na kaulimbiu “Kuongeza Ufanisi wa Majadiliano na Ushindani wa Mauzo ya Nje kwa Ustawi wa Uchumi” limehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
http://SERIKALI BEGA KWA BEGA NA WAFANYABIASHARA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO