DAR ES SALAAM.
Mkuu wa Chuo cha Taifa Utalii (NCT), Kampasi ya Bustani Jijini Dar es Salaam Dkt. Frolian Mtey, amesema kuwa Chuo hicho kimejipanga katika kuhakikisha kinatoa elimu bora na mafunzo stahiki kwa vijana wa kitanzania na kuimarisha mifumo ya Kidijitali ili wahitimu wake waweze kushindana kikamilifu kwenye soko la ajira Duniani
Dkt. Mtey ameyasema hayo katika Kongamano la nne la wanataaluma la kuwakutanisha wadau wa sekta ya Utalii, lililofanyika leo Disemba 5, 2025, Chuoni hapo katika Kampasi ya Bustani Jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikiendeleza jitihada zake za kuunga mkono maendeleo katika sekta ya utalii na kuwataka wahitimu hao kuwa waadilifu na kuwajibika kwenye maeneo yao ya kazi, kwani ulimwengu unahitaji uwajibikaji unaoheshimu tamaduni za watu.
“Maarifa ambayo mmepata hapa ni msingi, lakini ubunifu wako, na Kujitolea kwa vitendo endelevu kutafafanua mustakabali wa ukarimu na utalii. Nyinyi ndio waanzilishi wa kidijitali na viongozi wa kesho“ amesema Dkt. Mtey.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi la Kimataifa( ILO,) Bi. Caroline Khamati Mugalla, amesema kuwa sekta ya ukarimu na utalii kutengeneza fursa za kazi zenye staha na kwamba Sekta hiyo hutoa mamilioni ya ajira, haswa kwa vijana na wanawake.
“Ni mahali ambapo ujuzi unaweza kukua, na kazi zinaweza kuongezeka. Ndio maana ILO ipo mstari wa mbele katika masuala ya kukuza programu za mafunzo.
“Tumeunga mkono mipango hii kwa miaka mingi kwa sababu tunaamini katika kuwekeza katika ukuzaji ujuzi, kusaidia kuunda kazi nzuri na kukuza ujumuishaji wa kijamii“ ameeleza Bi. Mugalla.
Aidha amewakumbusha wahitimu hao kazi watakazofanya zina uwezo mkubwa wa kuunganisha watu, kuweka kumbukumbu, na kujenga na kujenga msingi utakaotumika kuwakaribisha wageni katika kupata huduma bora kwenye maeneo mbalimbali.
Naye mhitmu aliyeshika nafasi yajumla kwa kupata alama za juu kwenye masomo yake Ernest Julius ameupongeza uongozi wa Chuo hicho na wakufunzi waliofanikisha kufaulu masoo yake na kuahidi kwenda kufanyiakazi yale yote aliyoyapata na kujifunza katika Chuo hicho.
PICHA NA; HUGHES DUGILO