Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mkutano wa COP29 kulipa hadhi ya kipekee suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia katika mjadala wa kuhamasisha upatikanaji fedha za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan. Amesema Takriban watu milioni 900 barani Afrika bado wanatumia nishati chafu katika kupika hivyo kusababisha ukataji miti, upotevu wa sinki za kaboni na vifo kutokana na magonjwa yanayohusiana na moshi.
Makamu wa Rais amesema kutokana na umuhimu wa suala hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua kinara wa nishati safi Barani Afrika. Hadi sasa tayari amezindua programu ya nishati safi ya kupikia ya kuwasaidia wanawake barani Afrika (Pan-African Women Clean Support Programme) inayodhamiria kuhakikisha nishati safi ya kupikia inatumika kama suluhu Barani, inayogharimu takriban dola bilioni 4 kwa mwaka hadi kufikia 2030. Amesema hivi sasa Tanzania inatekeleza mkakati utakaohakikisha upatikanaji wa nishati safi, salama na nafuu ya kupikia kwa asilimia 80 ya kaya zote ifikapo 2034.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema Mkutano wa COP29 unapaswa kuhakikisha ahadi za fedha zilizotolewa zinatekelezwa kwa kufanya maamuzi ambayo yatasaidia upatikanaji wa fedha kwa nchi kulingana na udharura na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha amesema kufanyika kwa mapitio ya malengo ya kukusanya dola bilioni 100 iliyokubaliwa mwaka wa 2009 ni fursa ya kuleta mabadiliko katika ufadhili wa mazingira kwa sababu yatakayokubaliwa yatatoa taswira ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa miaka ijayo. Ameongeza kwamba ufadhili wa mazingira ni wajibu na haki kama ilivyokubaliwa katika Makataba wa Paris. Ametoa wito kwa COP29 kuimarisha mfuko wa Maafa ili kuhakikisha fedha hizo zinaleta maana na kwenda sambamba na mafaniko yaliyopatikana katika COP28 Dubai.
Makamu wa Rais amesema bado masoko ya biashara ya kaboni hayajaainishwa vema ikiwa ni pamoja na ukosefu wa taarifa zinazowezesha kushiriki kwa manufaa katika biashara hiyo hali inayopelekea nchi kukosa malipo yanayostahili.
Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuunga mkono juhudi za kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari zake. Amesema kama yalivyo mataifa mengine yanayoendelea, Tanzania pia inatumia rasilimali zake za ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayochochea nishati safi, miundombinu ya usafirishaji rafiki kwa mazingira, mifumo ya tahadhari iliyoboreshwa pamoja na udhibiti wa taka.
Amesema Tanzania imedhamiria kulinda na kuhifadhi bahari na misitu ambapo ina jumla ya eneo la hekta milioni 48.1 za hifadhi za misitu na makadirio ya uwezo wa kuhifadhi kaboni sawa na 2% ya jumla ya kaboni duniani. Vile vile uwepo wa ukanda wa pwani wa kilomita 1,424 na eneo la bahari la kilomita za mraba 64,500 ambayo inatoa fursa kubwa kwa uchumi wa bluu.
Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) kwa mwaka 2024 unaenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Mshikamano katika kujenga dunia ya kijani” inayolenga kuhimiza nchi wanachama kuungana na kutekeleza kwa pamoja juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.