Na Mwandishi Wetu, Liwale
SHIRIKA la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), limesema linatarajia kutumia mbinu ya uzio wa dawa ya harufu, mizinga ya nyuki na mabati yenye kelele kuzunguka shamba ili kuweza kudhibiti tembo waharibifu wa mazao ya wakulima wilayani Liwale mkoani Lindi.
Hayo yameainishwa na Mtaribu wa GIZ wilayani Liwale, Deborah Missana wakati akizungumza na waandishi wa habari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), ambao waliotembelea vijiji vinne kati ya 11 vinavyotekeleza Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.
Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori unatekelezwa katika Ukanda wa Ruvuma ukihusisha vijiji 30 vya Wilaya ya Liwale, Tunduru na Namtumbo.
Akifafua mbinu hizo Missana amesema mradi umetekelezwa katika vijiji 11 wilayani Liwale, ambapo GIZ imetoa mafunzo kwa wananchi zaidi 1,000 kutengeneza dawa yenye harufu ambayo inazungushwa kwenye shamba na kuzuia tembo kuingia katika mashamba ya korosho, ufuta, mpunga, alizeti na mengine.
Mratibu huyo ametaja vijiji vinavyonufaika na mradi huo wilayani Liwale ni Turuki, Kitogoro, Mtawatawa, Mtawango, Nanjegeja, Chimbuko, Mkutano, Ngumbu, Nahoro, Naluleo na Kimbemba
“Mradi umefamikiwa kufundisha njia mbadala ya utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ambapo hapa Liwale tumefundisha wananchi zaidi 1,000 kutengeneza dawa ya harufu ambayo imetumika kudhibiti tembo wakorofi,” amesema.
Amesema walianza kutoa mafunzo kwa maofisa ugani wa vijiji 11 na wakulima viongozi ambao walitoa mafunzo kwa wakulima wote, hivyo kurahisisha kazi hiyo.
Missana amesema mbinu hiyo imeonekana kuwa na mafanikio pamoja na kwamba wakulima wanakabiliwa na changamoto ya gharama za kununua vifaa husika.
Amesema wanachoweza kushauri kwa sasa ni wakulima kulima kilimo cha bega kwa bega, ili kupunguza gharama, huku wakizingatia uwekaji wa dawa ya harufu katika kipindi sahihi.
Mratibu huyo amesema kwa sasa wapo katika utekelezaji wa mbinu ya pili ambayo ni kutengeza uzio wa mizinga ya nyuki ambapo utafiti umeonesha tembo hapatani na nyuki.
Missana amesema hadi sasa wameshatoa mizinga 100 wilayani Liwale, huku lengo likiwa ni kutoa mizinga 310 ambayo itaweza kusaidia kukabiliana na changamoto ya tembo katika mashamba ya wakulima.
“Katika mbinu hii tutaweza kupiga ndege wawili kwa jiwe moja, kwani tembo atafukuzwa na wakulima watapata asili na kupata kipato,” amesema.
Missana amesema GIZ inatarajia kutengeneza uzio wa mabati katika mashamba hasa msimu wa mwaka ujao, hali ambayo itawafanya tembo wasiingie kula mazao ya wakulima.
“Tembo ni mnyama ambaye hapendi kelele, hivyo huu uzio wa mabati utatumika kuwafukuza na matokeo yake tutaona wakulima wakilima na kuweza kuvuna mazao mengi,” amesema.
Akizungumzia mbinu ya kutumia dawa ya harufu, Ofisa Ujirani Mwema kutoka TAWA, Aloyce Assenga alisema anaipongeza GIZ kwa kuja na dawa ya uzio wa harufu ambao unadaiwa kuwa na matokeo chanya katika mradi.
“Dawa ya harufu imeonesha matokeo chanya, hivyo sisi TAWA tutaendelea kuunga mkono, kwani inaonekana kukubalika. Lakini pia mbinu ya kutumia michoro imeonesha kuleta mabadiliko,” amesema.
Kwa upande wake Ofisa Kilimo Wilaya ya Liwale, Anthony Kawishe amesema mbinu ya matumizi ya dawa ya harufu imeweza kutoa matokeo chanya na wao kama wasisimizi wa sekta ya kilimo wanaunga mkono.
“Uzio wa harufu umekuwa na matokeo chanya katika vijiji vya mradi kwa tembo kuondoka, hivyo uzalishaji ukongezeka,” amesema.
Amesema kupitia mradi huo wameweza kupata Shirika la Maendeleo la Uswiss (Swiss Aid), ambao wamekuja na elimu ya shamba darasa kwa kufauta mbinu za kilimo ikolojia kwa kutumia viautilifu na mbolea za asili.
Amesema kupitia mafunzo hayo vijiji husika viliunda vikundi 24 vyenye wakulima zaidi ya 250 ambao wamekuwa wakitekeleza kilimo ikolojia.
“Swiss Aid imetoa vifaa vyote vya kilimo ikolojia kama keni za kumwagilia maji, mbegu mbalimbali na vingine muhimu,” amesema.
Amesema wao kama maofisa ugani wanaendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha wakulima wao wanaendelea kunufaika nao baada ya mradi kumalizika.
Kawishe amesema viuatilifu vinavyotumika katika kilimo ikolojia vinatengenezwa kwa kutumia tangawizi, pilipili, vitunguu saumu na nyinginezo.
Mkulima na Mkazi wa Turuki, Mariam Mtopeka ameomba serikali na wadau wengine kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo kwani wanaowaongezea umaskini.
Mariam amesema wakulima wengi wa kijiji cha Turuki wanalima katika eneo la Kitope, lakini wanagawana na tembo, hivyo kuiomba Serikali iweke nguvu kubwa.
“Sisi kipindi cha kilimo hatulali, kwani tembo wamekuwa hatari kimaisha na kwenye kilimo, hatuna uhakika wa kuvuna. Mfano kipindi hiki cha korosho anakula mabibo na akiona yapo juu anavunja mti ili kupata,” amesema.
Pia Asia Linachi, Amir Mikunya Zainabu Kimile na Rukia Salimu wa kijiji cha Turuki wameeleza kuwa mradi wa GIZ ina tija, ila nguvu zaidi inahitajika kudhibiti tembo.