Home LOCAL MBINU MPYA YA KUWADHIBITI TEMBO YAONESHA MWELEKEO WA MAFANIKIO SAME

MBINU MPYA YA KUWADHIBITI TEMBO YAONESHA MWELEKEO WA MAFANIKIO SAME

Wananchi wafanikiwa kuvuna mazao yao, waishukuru Serikali

Na Beatus Maganja, Kilimanjaro

Hatimaye mbinu mpya ya kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo iliyobuniwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA ambayo tayari imeanza kutumika kuzuia tembo kuleta athari kwa maisha na mali za wananchi waishio wilaya za Same na Mwanga Mkoani Kilimanjaro imeanza kuonesha mwelekeo wa mafanikio baada ya wananchi kukiri kuwasaidia.

Katika nyakati tofauti, wakizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika ziara iliyofanywa na TAWA wilaya za Same na Mwanga Oktoba 31, 2024 Mkoani Kilimanjaro wananchi hao wameishukuru TAWA kwa elimu waliyowapa, umoja na ushirikiano wanaoutoa kwao katika kukabaliana na changamoto ya tembo jambo ambalo wanakiri limewasaidia kujilinda dhidi ya madhara yatokanayo na wanyamapori hao na pia kupata mavuno Kwa wakati.

“Tunashirikiana na watu wa TAWA vizuri sana na maelekezo wanayotupa kuhusiana na tembo ni mazuri sana, ni kweli hawa tembo wanasumbua lakini Kwa kushirikiana inawezekana kuwakabiri” amesema Karanga Mhina mkazi wa Kijiji cha Kitamri kilichopo Kata ya Stesheni wilayani Same

“Tunawashukuru sana hawa TAWA Kwa kutupa elimu ya kufukuza hawa tembo, zamani sisi tulikuwa hatulimi ila sasa hivi tunalima lakini pia wametupa vifaa vizuri sana, mabomu baridi ya kufukuza tembo na sasa hivi tukiwafukuza angalau tunavuna” ameongeza Mhina

Naye Afisa Uhifadhi wa TAWA kutoka kituo cha Ruvu Same Yohana Mgalula amesema kutokana na ukubwa wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo inayowakabili wananchi wa ukanda huo, Mamlaka kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali walikuja na mbinu ya kuwashirikisha wananchi Kwa kuhamasisha uundwaji wa vikundi jamii vya ulinzi wa mazao ambavyo anakiri kuwa vimeleta tija na ufanisi Kwa kiwango kikubwa.

Mgalula amesema baada ya kuunda vikundi hivyo, Mamlaka ilivipatia elimu ya kujikinga dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori hao sambamba na mbinu za kuwafukuza hasa pale wanapovamia makazi au mashamba yao. Ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi ikiwemo vuvuzela, filimbi,tochi zenye mwanga mkali jambo ambalo limeviwezesha vikundi hivyo kushiriki kwa zaidi ya asilimia 90 kuwadhibiti wanyamapori hao bila uwepo wa Askari wa TAWA.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amepongeza mwitikio wa wananchi hao kushirikiriana na Serikali katika kukabaliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu na kusisitiza kuwa TAWA itaongeza kasi ya kuendelea kuwapa elimu pamoja na mbinu mbalimbali za kukabaliana na wanyamapori hao sambamba na kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia katika utekelezaji wa jukumu hilo.

“TAWA tutaendeleza kasi ya kuwapa elimu wananchi katika maeneo mbalimbali yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini, jukumu hili tutalifanya Kwa nguvu kubwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama” amesema Maganja.

Previous articleWAJUMBE WA BODI NIRC WAAAHIDI USHIRIKIANO KWA MWENYEKITI MPYA WA BODI
Next articleMAANA YA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN KUIFUNGUA NCHI.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here