Tanzania na Urusi zimekamilisha mkutano wa kwanza wa tume ya pamoja ya ushirikiano wa biashara na uchumi, ambapo pande hizo zimesaini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Mkutano huo umefanyika jana jijini Dar es Salaam na umejumuisha shughuli mbalimbali, ikiwemo mkutano wa wataalamu, mkutano wa tume pamoja, na kongamano la uwekezaji, kabla ya kutia saini makubaliano hayo na waheshimiwa mawaziri.
Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Urusi, Mhe. Maxim Reshetnikov, wameeleza kwamba nchi zao zinachukua mkondo wa uhusiano wa biashara na uchumi. Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa miongo sita ya uhusiano kati ya Tanzania na Urusi imekuwa imara kisiasa na kiutamaduni, ikileta manufaa makubwa katika nyanja za elimu, sayansi, na teknolojia.
Makubaliano yaliyotiwa saini yanazingatia kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na viwanda na biashara, fedha, nishati, kilimo, elimu, sayansi na teknolojia, uchukuzi, afya, na habari, mawasiliano na teknolojia ya habari. Aidha, maliasili, utalii, utamaduni, na michezo ni maeneo mengine ya ushirikiano yaliyofikiwa.
Waziri Reshetnikov alisisitiza kuwa Urusi inaona Tanzania kama mmoja wa washirika muhimu katika ukanda wa Afrika, na kwamba lengo lao ni kuifanya Tanzania kuwa mshirika wa kimkakati katika masuala ya biashara na uchumi.
Mkutano huo umehudhuriwa na wageni mbalimbali, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Pindi Chana, na Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Exaud Kigahe, pamoja na Mhe. Injinia Meryprisca Mahundi. Mkutano wa wataalamu uliokuwa na wajumbe kutoka pande zote mbili uliongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Tausi Mbaga Kida kwa upande wa Tanzania, na Bwa. Pavel Kalmychek, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Uwili kutoka Wizara ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Shirikisho la Urusi.