Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeelezea kuridhishwa kwake na mwitikio mkubwa wa wananchi katika zoezi la uandikishaji wa daftari la wakazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mkoani Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea taarifa ya zoezi hilo leo, Jumanne Oktoba 22, 2024, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ambaye pia ni mlezi wa chama hicho mkoani Dar es Salaam, amepongeza viongozi wa CCM na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano wao katika kufanikisha zoezi hilo.
Makalla alibainisha kuwa uandikishaji huo umefikia asilimia 96.7, akieleza kuwa hii ni ishara ya faraja kwa CCM, hasa kwa kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha taifa. “Niwapongeze viongozi wetu wa CCM kuanzia ngazi ya mkoa hadi mabalozi, pamoja na wafuasi wa chama na wananchi wa mkoa mzima kwa ushirikiano wao wa hali na mali katika kufanikisha zoezi hili,” alisema.
Utekelezaji wa Ilani ya CCM Ulichochea Mwitikio Mkubwa
Makalla alifafanua kuwa mwitikio mkubwa wa wananchi katika kujiandikisha unatokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo imeleta maendeleo makubwa kwenye maeneo ya huduma za afya, elimu, na miundombinu. “Wananchi wameona miradi inatekelezwa kwa vitendo. Zahanati, madarasa, na vituo vya afya vimejengwa vijijini na vitongojini, na hii imesaidia kuchochea ari ya wananchi kushiriki katika zoezi hili muhimu,” alieleza Makalla.
CCM Kujitafakari Endapo Itapoteza Eneo Lolote
Hata hivyo, CPA Makalla alisisitiza kuwa CCM itaheshimu matokeo ya uchaguzi huo, hata kama itapoteza katika baadhi ya vijiji, vitongoji, au mitaa. Alisema kwamba chama hicho kitajitathmini na kujipanga upya, ili kuelewa sababu ya kushindwa, kama hatua ya kujiimarisha kwa ajili ya chaguzi zijazo.
“Kama tukipoteza katika eneo lolote, huo utakuwa wakati muafaka wa kujitafakari. Tunapaswa kujua ni kwa nini tumeshindwa, na tujitayarishe vyema kwa uchaguzi ujao,” alisema.
Maandalizi Yaleta Taswira ya Ushindi wa Kishindo
Makalla alihitimisha kwa kusisitiza kuwa CCM haitegemei mbeleko ili kushinda, bali ushindi wake unajengwa na maandalizi thabiti na kazi nzuri inayofanywa na viongozi wa chama pamoja na jumuiya zake. Alisema takwimu kutoka ndani ya chama na zile za Wizara ya Tamisemi zinatoa matumaini makubwa ya ushindi mnono katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa.