Home SPORTS MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA YAMEKUWA TISHIO NCHINI

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA YAMEKUWA TISHIO NCHINI

Na: WAF – Bugando, Mwanza

Watanzania wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani, kisukari na shinikizo la juu la damu kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo Oktoba 20, 2024 akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko kwenye mbio za ‘Bugando Health Marathon’ zenye lengo la kuchangia watoto wenye saratani ambazo zimeratibiwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa kushirikiana na wadau.

“Mbio hizi zinalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuchangia watoto wenye saratani wanaopata huduma katika hospitali hii, lengo likiwa ni kufikia Bilioni Moja ili kuwahudumia watoto zaidi ya 300 wenye saratani mbalimbali na kuendelea kupata huduma za matibabu katika hospitali hii,” amesema Waziri Mhagama

Amesema, tunapaswa kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya viungo pamoja na kukimbia, kula vyakula vyenye mbogamboga, kupunguza matumizi ya chumvi, sukari pamoja na mafuta kwenye vyakula, kwani magonjwa haya yameendelea kuongezeka ikiwemo saratani, kisukari pamoja na magonjwa ya figo na kutibu magonjwa haya ni gharama kubwa.

Aidha, Waziri Mhagama amesema idadi ya watoto wanaougua ugonjwa wa saratani imeendelea kuongezeka kutoka watoto 50 hadi 300 kwa mwaka, katika hospitali ya Bugando na wengi wao wanaougua saratani wanatoka katika familia duni hali inayosababisha kushindwa kugharamia matibabu yao.

Waziri Mhagama ametoa wito kwa taasisi zote nchini, pamoja na wadau wa maendeleo wa Sekta ya Afya kuendelea kuiunga mkono hospitali ya Bugando kwa kuchangia mahitaji mbalimbali ya wagonjwa kila wakati hasa katika mbio za marathon zitakazofuata, kwani majitoleo yao si bure mbele za Mungu.

” Idadi ya wagonjwa wa saratani nchini imekuwa ikiongezeka baada ya Serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye miundombinu ya afya hasa maabara za uchunguzi wa magonjwa zenye vifaa vya kisasa ambavyo vinaweza kutambua wananchi wengi wanaogundulika mapema na kupatiwa tiba,” amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama ametoa takwimu za saratani kwa kueleza kuwa saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa akina mama kwa asilimia 24.2 tezi dume asilimia 10 saratani ya matiti 10, koo asilimia 7.9, utumbo mpana asilimia 4.9 hivyo wanaougua ugonjwa wa saratani hapa nchini ni asilimia 42.4

Previous articleMCHECHU ACHANGISHA SH.117.8.MILIONI UJENZI WA KANISA NAIBILI
Next articleMFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA MKOMBOZI KWA MKULIMA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here