Na Veronica Mheta, Arusha
Vyama vya Ushirika Nchini vimeendelea kushauriwa kutumia Mfumo wa Kidigitali wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika ( MUVU) ili kuwawezesha watendaji kuendesha shughuli zao kiufasaha,kurahisisha upatikanaji wa taarifa,kuhifadhi taarifa hizo na kuweza kuwasilisha taarifa hizo sahihi kwa mamlaka stahiki kwa wakati.
Mifumo ya manunuzi ya bidhaa kwa kupitia vyama vya ushirika Ile ya TMX na Stakabadhi ghalani(WRRB) ni mifumo inayomnufaisha mkulima na kuongeza uwazi,inawezesha minada ya kidigitali,uhuru wa kuamua na kuona bei zilivyo kwenye masoko,uhakika wa upatikanaji wa masoko pamoja na kuchochea ushindani wa mazao.
Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Alliance for Global Goals Foundation(A.G.G.F),Dk Nsiande Urasa wakati akikabidhi msaada wa kompyuta kadhaa kwa baadhi ya vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) vinavyojishughulisha na mazao mchanganyiko ikiwemo kahawa,katika ofisi za chama kikuu jijini Arusha.
Amesema hapo awali Waziri mwenye dhamana ya ushirika,Waziri wa Kilimo Mohamed Bashe amekuwa akitamani kuwe na mashirikiano baina ya AMCOS na SACCOS au SACCOS ndani ya AMCOS na kusema mashirikiano ni mawasiliano na mawasiliano yanaweza fanyika kwa kutumia teknolojia mfano kompyuta.
Msaada huo umetolewa kwa kuzingatia misingi ya ushirika, ule wa kujali jamii na ule wa mashirikiano miongoni mwa wanaushirika.
Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Arusha, Robert George amesema ufadhili huo wa kumpyuta utasaidia vyama vya ushirika kufanya kazi kwa ufanisi katika kuhakikisha utunzaji wa kumbukumbu ulio sahihi unakuwepo kwa kutumia mifumo mbalimbali ya serikali kwa vyama vya ushirika nchini kwani awali vyama hivyo vilikuwa vikitunza kumbukumbu kwa njia ya makaratasi na kuwa ni rahisi kwa taarifa muhimu kupotea.