Home LOCAL WAKULIMA KUNUFAIKA NA ZAO LA TUMBAKU -DKT PHILIP MPANGO

WAKULIMA KUNUFAIKA NA ZAO LA TUMBAKU -DKT PHILIP MPANGO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Kilimo kuendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha wakulima wa zao la tumbaku wananufaika na zao hilo pasipo unyonyaji kutoka kwa makampuni na watu binafsi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Magiri akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Uyui mkoani Tabora. Amesema ni muhimu hatua kuchukuliwa ili kulinda zao la tumbaku pamoja na kuwalinda wakulima ikiwemo kudhibiti mfumo wa ulanguzi (kangomba) na kufuatilia makampuni ambayo yanayodaiwa na wakulima. Aidha amesisitiza kufuatwa kwa utaratibu uliowekwa na serikali katika utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa mazao ikiwemo zao la tumbaku.
Aidha ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Uhamiaji kuweka mkazo katika kudhibiti wahamiaji haramu katika wilaya hiyo pamoja na kuongeza kasi ya utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa maeneo ya mipakani.

Pia ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutatua changamoto ya mawasiliano katika Wilaya ya Uyui ili kurahisisha shughuli za kiuchumi wilayani humo.

Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Wilaya hiyo kuishi katika misingi ya maadili na kuachana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na ukatili kwa watoto. Amesema Serikali imejenga miundombinu ya elimu ya kisasa hivyo ni vema kutumika kwa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ikiwemo walemavu.

Makamu wa Rais akiwa Wilayani Uyui ameweka jiwe la msingi ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui unaogharimu shilingi milioni 700 ambao unatarajiwa kutumika kama chanzo cha mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo kupitia ukodishaji.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesisitiza azma ya serikali ya kutoa ruzuku kwa mkulima moja kwa moja ili kuondoa urasimu na matumizi yasiyo sahihi ya fedha hizo. Amesema kwa sasa wakulima wa zao la tumbaku wataanza kuingia mikataba ya muda mrefu ya miaka mitatu na makampuni ya ununuzi ili kuwaondolea mzigo wa ulipaji madeni wanaopata wakulima katika msimu mmoja.

Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Tabora kwa lengo kukagua shughuli za maendeleo, kuzindua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
09 Oktoba 2024
Uyui – Tabora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here