Ujumbe kutoka Chama cha Wachimbaji Wadogo kutoka Kenya umevutiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa hatua kubwa iliyopiga katika sekta ya madini hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 7 Oktoba na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Kenya (ASMAK),Bw Patrick Ligami alieongoza ujumbe wa watu wawili walipotembelea Kijiji cha STAMICO na Wadau Wake kwenye maonesho ya Madini yanayoendelea hapa Geita.
“Nimefurahishwa sana na jinsi STAMICO ilivyopiga hatua kubwa kwa kuwasaidia wachimbaji wadogo”alisema.
Alisema kuwa ujumbe wa watu 12 umetumwa na Serikali ya Kenya kuja kujifunza kwenye maeneo mbalimbali kwenye maonesho haya.
Alisema kuwa ujumbe kutoka Serikali ya Kenya utatembelea makao makuu ya STAMICO baada ya maonesho haya ili kujifunza namna sekta hii ya madini na hasa wachimbaji wadogo inavyoendeshwa.
Ujumbe huo ulivutiwa na wazo la Kijiji cha STAMICO na Wadau Wake kuwa nao eneo moja kwenye maonesho haya.
Ujumbe huo ulivutiwa pia na teknolojia rahisi ya wachimbaji wadogo ambayo amesema itawafaa sana nchini Kenya.
Aliupongeza uongozi wa Shirika kwa juhudi hizo na kutoa rai kuwa liendelee kuwalea wachimbaji wadogo ili Kenya iweze kujifunza.
Vikundi ambavyo vimealikwa na STAMICO na kushiriki ndani ya banda moja ni pamoja na FEMATA,TAWOMA, TAMAVITA,FDH,Tanzania Youth Miners na Chama cha Wachimbaji Geita (GEREMA).
Wengine ni pamoja na kikundi cha Wanawake na Samia Geita na Chama cha Wanawake Geita (GEWOMA).