Ujumbe kutoka Comoro, ukiongozwa na Gavana wa visiwa vya Ngazija, Mheshimiwa Mze Mohammed Ibrahim, umetembelea shamba la kilimo la Ubena Estate lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, mkoani Pwani. Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu wa ufugaji wa mifugo bora inayoweza kushindana katika soko la nyama kati ya Tanzania na Comoro. Pamoja na Gavana, ujumbe huo ulijumuisha wataalamu wa biashara na kilimo kutoka Comoro waliokuja kujifunza mbinu za ufugaji wa kisasa.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulijifunza namna Tanzania inavyoandaa wataalamu wa mifugo kupitia taasisi mbalimbali. Kwa upande wa Comoro, waliweka wazi kuwa hawana taasisi zinazotoa mafunzo kwa sekta ya mifugo, jambo ambalo limekuwa changamoto kwao. Ujumbe huo ulieleza kuwa mifugo inayopelekwa Comoro kwa ajili ya kuchinjwa inakumbwa na magonjwa, hivyo mifugo ya maziwa haiwezi kustawi.
Wataalamu wa Tanzania walitoa ushauri kwa Wakomoro kuwa ili kufuga kwa mafanikio, wanapaswa kuwa na taasisi zinazotoa mafunzo ya mifugo na kufanya tafiti kuhusu magonjwa yanayowakabili mifugo yao. Pia, waliwashauri kununua mifugo kutoka maeneo yenye hali ya hewa inayofanana na Comoro ili kuzuia matatizo yanayojitokeza kutokana na tofauti za kijiografia.
Ujumbe huo pia ulitembelea mashamba ya mkonge ya Ubena Estate, yenye ukubwa wa hekta Elfu nne, ambapo waliona ng’ombe wa nyama na maziwa zaidi ya 1,400. Walijifunza hatua za uzalishaji wa nyuzi za mkonge na uchakataji wa zao hilo. Mkurugenzi wa Ubena Estate, Bwana Naweed Y. Mulla, aliwaeleza kuhusu aina mbalimbali za ng’ombe wanaofugwa shambani hapo na umuhimu wa kilimo cha mkonge katika sekta ya uchumi.
Kwa niaba ya ujumbe kutoka Comoro, Gavana Mze Mohammed Ibrahim aliishukuru Tanzania, hasa serikali ya Mkoa wa Pwani na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, kwa ushirikiano na elimu waliyoipata kuhusu ufugaji. Aliahidi kuwa Comoro itaendeleza ushirikiano na Tanzania ili kuboresha tasnia ya mifugo katika nchi yake.