DAR ES SALAAM.
KATIBU Mkuu wa Tamisemi Profesa Riziki Shemdoe ametoa siku moja kwa maafisa wa Utumishi wa majiji,wilaya pamoja na manispaa zote nchini kukamilisha mchakato wa upandishaji wa madaraja na vyeo kwa watumishi wao ikiwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Profesa Shemdoe alitoa agizo hilo kwenye Ofisi za halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kujionea namna zoezi la upandishwaji wa vyeo na madaraja mbalimbali na kutoa msisitizo kwa halmashauri nyingine kuhakikisha wanamaliza mchakato huo haraka iwezekanavyo.
“Sintokuwa tayari nipoteze kazi kwa sababu ya uzembe wa mtu, kila halmashauri inapaswa kukamilisha kazi hiyo ifikapo kesho, nasisitiza kuwa wale ambao bado hawajakamilisha kazi hiyo hadi hivi sasa kuhakikisha wanaliza kabla ya hatua zingine” alisisitiza Profesa Shemdoe.
Aidha Prof. Shemdoe aliipongeza halmashuri hiyo kwa kufanyakazi usiku na mchana na kuweza kukamilisha zoezi hilo kwa kiasi kikubwa huku akiipongeza idara ya utumishi wa halmashauri hiyo kwa kuwezesha kufanyika kwa mchakato huo.
Kwa upande wake Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Jiji hilo Bi. Bernadetha Mwaikambo, amesema kuwa mpaka sasa wameweza kuwafikia jumla ya watumishi 2555 kati ya 2625 waliopandishwa vyeo na madara mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo nakwamba watumishi hao wote tayari wameshaingizwa katika mfumo ambapo watumishi waliosalia wapatao 70 hakuweza kuingizwa kwenye mfumo kutokana na changamoto mbalimbali.