Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akionyesha Cheti cha Utumishi Bora alichokabidhiwa Mkurugenzi wa Kitengo Cha Sheria Bw. Merick Luvinga kwenye Banda lililopo ofisi za Wizara jengo la NHIF, Mjini Dodoma mapema leo 18 Juni. |
Na: Catherine Sungura, DODOMA.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kesho 19 Juni, Mwaka huu anatarajiwa kusikiliza kero na malalamiko ya watumishi wa Wizara Kwenye ukumbi wa Wizara mji wa Serikali Mtumba.
Akizungumza wakati wa kuzindua maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mapema leo mjini hapa, alisema kuwa katika kuadhimisha wiki hiyo, atatumia wasaha huo wa kukutana na watumishi ili kusikiliza kero zao mbalimbali kwa lengo la kuzifanyia kazi.
Katika maadhimisho hayo mwaka huu ni “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata Katika mazingira ya mgogoro.
Aidha, Dkt. Dorothy Gwajima ameweza kumkabidhi Cheti Cha Utumishi Bora Mkurugenzi wa Kitengo Cha Sheria, Bw.Merick Luvinga Kwenye Banda lililopo ofisi za Wizara jengo la NHIF.
Dkt.Gwajima amesema Wizara imempatia Cheti hicho kilichosainiwa na yeye pamoja na Katibu Mkuu, Prof. Abel Makubi ikiwa ni kutambua kazi nzuri anayofanya wizarani pamoja na Taasisi zingine kwani wameshapokea barua mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi nyingine ambazo amekua akifanya nao kazi za kumpongeza Mkurugenzi Luvinga .
Mwisho.