Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Tunduru waliojitokeza kwa maelfu kumsikiliza kwenye mkutano mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa CCM, Tunduru Mjini, tarehe 26 Septemba 2024.
Pamoja na kuwashukuru kwa mwitikio wao mkubwa wa kuja kwa wingi kwenye mkutano huo wa hadhara, Rais Dkt. Samia alitumia fursa hiyo kuendelea kutoa wito kwa wananchi wa Tunduru, mkoa wa Ruvuma na nchi nzima kwa ujumla, kujiandaa kikamilifu kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba, mwaka huu.
Katika wito huo, Mhe. Rais Dkt. Samia amewataka Watanzania kutumia uchaguzi huo kuchagua viongozi bora, wenye sifa ya kuwa watumishi wa wananchi, ambao wataweka maslahi ya wananchi na nchi mbele, ikiwemo kulinda amani na utulivu kwa ajili ya maendeleo ya taifa, badala ya kutanguliza mambo binafsi.
Kabla ya kuhutubia mkutano huo wa hadhara uliokuwa na hamasa na bashasha kubwa ya kumsikiliza, Mhe. Rais Dk. Samia alipata fursa ya kuzindua jengo la soko la madini ya vito na dhahabu, lililojengwa kwa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, wilayani Tunduru.
Aidha, kabla ya hapo, Mhe. Rais Dkt. Samia alipata fursa ya kuzungumza na wananchi katika maeneo ya Likola, Rwinga na Mchomoro, wilayani Namtumbo, kisha akazungumza na wananchi wa Tarafa ya Matemanga, wilayani Tunduru, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Mkoa wa Ruvuma. Katika maeneo yote hayo, alifurahishwa jinsi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025 inavyotekelezwa kwa vitendo kuwahudumia wananchi.