Maelfu ya wananchi wa Mji wa Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa, walijitokeza kumlaki na kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipowasili eneo hilo kwa ajili ya kuzindua mradi muhimu wa barabara na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari, leo tarehe 25 Septemba 2024.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Samia alizindua barabara ya Mbinga – Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66, ambayo imeshakamilika kwa kiwango cha lami. Aidha, alihudhuria kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay.
Barabara hiyo ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha shughuli za uchumi na uzalishaji, hasa katika maeneo yanayojulikana kwa kilimo cha kahawa na mahindi.
Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo uliogharimu Shilingi bilioni 122.76, umesimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS).
Katika kutekeleza mradi huu, kiasi cha Shilingi milioni 637.4 kilitumika kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi, kwa mujibu wa sheria.
Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay ni sehemu ya barabara kuu ya ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) yenye jumla ya urefu wa kilometa 826, ikianzia Mtwara hadi Mbamba Bay. Pia inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Mtwara pamoja na Mkoa wa Mbeya na nchi jirani ya Malawi kupitia Ziwa Nyasa.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia kabla ya kuhitimisha ziara yake wilayani Nyasa, kwa kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Bandari, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay. Bandari hii, itakapokamilika, inatarajiwa kuwa moja ya nyenzo muhimu za kuchochea shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi, sambamba na kuwa kiungo muhimu cha usafirishaji wa bidhaa na watu katika Ziwa Nyasa, nchini Tanzania na nchi za jirani, hususan Malawi.