Home LOCAL MHE. ZAINABU TSC ENDELENI KUSIMAMIA MAADILI YA WALIMU

MHE. ZAINABU TSC ENDELENI KUSIMAMIA MAADILI YA WALIMU

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Mhe. Zainabu Katimba akifungua  mafunzo ya siku mbili ya walimu kwa niaba wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa. 

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Prof. Masoud Muruke amizungumza katika mafunzo hayo.

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Na, Mwandishi wetu_TSC Dar es Salaam

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Mhe. Zainabu Katimba ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu(TSC) kuendeleza jukumu lake la msingi la usimamizi wa utumishi na Maadili ya Walimu.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Septemba, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa niaba wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati za Wilaya za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutekeleza majukumu yao.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwa na walimu wenye kujituma na wanaozingatia maadili ya kazi yao kwa ajili ya kuwalea Watoto kwa usahihi na hivyo kuboresha elimu nchini.

Mhe. Zainabu aliwataka washiriki kutumia mafunzo yenye mada zinazohusu Muundo na Majukumu ya Tume, Majukumu ya Kamati za Wilaya pamoja na taratibu katika ushughulikiaji wa mashauri ya nidhamu na Rufaa kwa Walimu kuwa chachu ya kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Tume na Serikali kwa ujumla

Alisema kuwa baada ya mafunzo ni vema wakatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo hatimaye watende haki kwa walimu kwa kujituma na kwa uaminifu mkubwa.

Naomba nirudie kuipongeza Tume kwa kazi nzuri mnayoifanya… Naomba sote kwa pamoja tuendelee kutekeleza kauli mbiu ya “Kazi iendelee”. Kauli mbiu hii naomba itekelezwe kwa ufanisi na uadilifu na sisi kama Serikali tutaendelea kuwa pamoja nanyi katika kuhakikisha kwamba tunatoa ushirikiano wa kutosha,” alisisitiza.

Aidha, Mhe. Zainabu alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuhakikisha kuwa, Wizara na Taasisi zinazosimamia Utumishi wa Walimu zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzipatia fedha, nyenzo na watumishi wenye ujuzi na weledi wa kutosha ili kuboresha Sekta ya Elimu Nchini.

Awali Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Prof. Masoud Muruke alisema kuwa Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati za Wilaya yanafanyika katika Kanda mbalimbali ambapo Kanda ya Kaskazini itahusisha ambapo mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, Kanda ya Mashariki inahusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Alisema kuwa kwa Kanda ya Kati ina mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora, Singida na Dodoma, Kanda ya Ziwa ina mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo ina mikoa ya Rukwa, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya.

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila alisema kuwa Walimu wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia, kwa juhudi zake za kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwakabili walimu ikiwemo za kuwapandishwa madaraja.

Aliwataka Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuhakikisha wafanyakazi kwa juhudi katika kumsaidia Rais katika usimamizi wa nidhamu, mashauri na madaraja kwa walimu kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.

 

Previous articleRAIS SAMIA: HONGERA MBINGA KWA UZALISHAJI MZURI WENYE USALAMA NA UHAKIKA WA CHAKULA
Next articleRAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA BANDARI YA MBAMBABAY

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here