Na: Damian Kunambi, Njombe.
Viongozi wa kata na vijiji wilayani Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kuthamini michango inayotolewa na wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuwapa nguvu ya kuendelea kuchangia zaidi sambamba na kuonyesha thamani ya michango yao.
Hayo ameyasema katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Ludewa Bakari Mfaume alipokuwa akikagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa katika kata mbalimbali za wilaya hiyo akiwa ameongozana na kamati ya siasa ya wilaya hiyo pamoja na wakuu wa idara za serikali ngazi ya wilaya ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 na kwa mujibu wa kalenda ya chama hicho.
Amesema wananchi wamekuwa wakihamasishwa kutoa michango ya nguvu kazi katika ujenzi wa miradi hiyo lakini thamani ya nguvu wanazochangia zimekuwa hazitambuliki kutokana na kutochukuliwa kwa uzito wake hivyo wanapaswa kupewa mrejesho baada ya kukamilika ujenzi huo na kuwapa pongezi pia.
Ameongeza kuwa wananchi wamekuwa wakipewa kazi ya kufyatua tofali, kukusanya mawe milimani, kuchota mchanga n.k hivyo kama viongozi wanapaswa kuthaminisha shuguli hizo wanazofanya wananchi katika fedha ili kujua wamechangia kwa kiwango kipi ikiwezekana baada ya ujenzi kuisha washukuriwe kwa michango yao kwani hii itawapa nguvu ya kujitoa zaidi.
“Wananchi wamekuwa wakijituma sana katika kuchangia shughuli hizi, tumekuwa tukisema tu wananchi nao wamechangia je! Ni kwakiwango gani? Viongozi mnapaswa kubadili nguvu kazi katika thamani ya pesa kwa mfano, wananchi wamefyatua tofali zilizotumika kujenga jengo zima mnapaswa kuangalia zimetumika tofali ngapi mnapiga hesabu endapo zingenunuliwa ingetumika kiasi gani cha fedha jibu mtakalopata hicho ndicho kiasi walichochangia wananchi na wanapaswa kushukuriwa”, Alisema Mfaume.
Sanjari na hilo pia amewataka wananchi kufuatilia kwa karibu uendeshwaji wa miradi hiyo na endapo wanapoona inaenda tofauti wanahaki ya kuhoji na kupewa majibu kwakuwa wao pia ni wadau wa maendeleo.
Aidha kwa upande wa katibu siasa na uenezi wa chama hicho ngazi ya wilaya Josaya Luoga amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia vyema majengo hayo na yanajengwa kwa ubora unaotakiwa ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesema wanapaswa kumjulisha mhandisi wa majengo kila hatua wanayofikia ili aweze kuja kutathimini ubora wa jengo hilo kabla hawajafika mwisho na kutoa ushauri.
“Kumekuwa na kawaida ya viongozi kujenga majengo kwa kiwango kikubwa ndipo wanawaita wahandisi waje kutathimini kitu ambacho kinaleta hasara pale inapoonekana hitilafu wakati jengo limesha nyanyuka, hivyo ili tuweze kujenga majengo bora tunapaswa kushirikiana na hawa wataalam ili kupata majengo ya uhakika zaidi”, Alisema Luoga.
Pia amewataka viongozi kuwa waaminifu wanapopokea fedha na vifaa vya kutumia katika majengo hayo kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwa wazalendo wa nchi yao na kuleta maendeleo yaliyo bora.
Kamati hiyo imeanza kwa kukagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Mbongo kata ya Manda vinavyojengwa na makundi ya Whatsapp ambayo ni ya wazawa wa wilaya ya Ludewa na kundi la wazawa wa kata ya Mbongo, jengo la mama na mtoto pamoja na zahanati Katika kijiji cha Ilela kata ya Luhuhu, zahanati ya kijiji cha Lifua kata ya Luilo pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu katika kata ya Nkomang’ombe.
Katika miradi hiyo yote mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ametoa mchango mkubwa kupitia mfuko wa jimbo pamoja na mchango wake binafsi.