Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua barabara ya Mbinga – Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Ruvuma, leo Septemba 25, 2024.
Ujenzi wa Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay (km 66) umesimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara – TANROADS chini ya Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd kutoka China na Mhandisi Mshauri kutoka SMEC International Pty Ltd kutoka Australia kwa gharama ya Shilingi Bilioni 122.76.
Katika utekelezaji wa barabara hiyo, Kiasi cha shilingi Milioni 637.4 kilitumika kulipa fidia kwa wananchi walioathirika na ujenzi kwa mujibu wa sheria.
Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay ni sehemu ya barabara kuu ya ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) yenye jumla ya urefu wa kilometa 826 inayoanzia Mtwara mpaka Mbamba Bay ambapo pia barabara hiyo inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Mtwara pamoja na Mkoa wa Mbeya na nchi Jirani ya Malawi kupitia Ziwa Nyasa.