Na: Alex Sonna,DODOMA.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri amelitaka Shirika la Viwango nchini (TBS) kufungua ofisi katika maneo ya Wilayani ili kuwapa elimu wananchi wengi jinsi ya taratibu za uthibitishaji ubora na usalama wa bidhaa na mifumo yake unavyoweza kupatikana.
Akizungumza leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa umma yaliyoandaliwa na TBS,Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuna haja ya TBS kufungua ofisi katika Wilaya na Kata ili kuwapa elimu na taratibu za uthibitishaji ubora na usalama wa bidhaa na mifumo yake.
Mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kuwapa walengwa uelewa kuhusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS), majukumu yake ikiwemo taratibu za uandaaji Viwango, Matumizi ya Viwango na faida zake, taratibu za uthibitishaji ubora na usalama wa bidhaa na mifumo yake, vifungashio, na usajili wa majengo yanayotumika kwa bidhaa za vyakula na vipodozi.
“TBS wamekuwa wakifanya kazi na sekta binafsi kuelewesha kuhusiana na masuala ya viwango mtakubalina TBS hawapo katika maeneo yote hawapo Wilayani ngazi ya kata na vijiji kwa hiyo ni muhimu wakawa na watu wa kuwasemea na kuwasaidia kuhusu masuala ya viwango.
“Niwakumbushe tu sisi Mkoa wa Dodoma na Kigoma tumekuwa kwenye ufadhili wa Danida na tunaendesha mabaraza ya biashara kwahiyo kupitia uwekezaji ni lazima tuweke mazingira vizuri,”amesema.
Hata hivyo,Shekimweri ameitaka TBS kuhakikisha inazisimamia bidhaa zenye ubora ili kwani ndizo ambazo zinahitajika katika soko.
“Hii inaenda kuongeza uwezekano na ufanisi wa viwanda katika maeneo ya uchakataji kwahiyo kila eneo lenye uzalishaji kwa sababu ya miundombinu ya barabara hizi kazi za kwenye masoko kuna ushindani bidhaa zenye ubora ndizo ambazo zitakubaliana na soko.
Pia amesema kuna haja ya TBS kusaidia maendeleo mara baada ya Tanzania kuingia uchumi wa kati ikiwa ni pamoja na tafsiri iweze kuonekana kwa wananchi.
“Kwa hiyo hoja hapa ni namna gani kupitia TBS maendeleao haya ya uchumi wa kati yapatikane na kuwatayarisha wazalishaji waelelewe umuhimu wa TBS .Ni kuhusisha sisi wataalamu ili tafsiri ya uchumi wa kati iweze kuonekana TBS tunaomba mtusaidie katika hili,”amesema.
Vilevile amewataka washiriki wa mafunzo hayo wayatumie vizuri ili kuweza kujua mambo mengi huku akiwakumbusha kusukuma gurudumu la maendeleo mbele kwa kukitumia kile ambacho wamefundishwa kwa vitendo.
“Nawapongeza TBS isiwe mara ya mwisho endeleeni kutoa mafunzo nategemea kutakuwa na marejeo ya mafunzo haya ili watu waweze kuendelea kupata maarifa matumaini yangu mtaendelea kuwasaidia watanzania,”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa TBS,Dkt.Athumani Ngenya amesema mafunzo haya yameandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa lengo la kutoa mafunzo ili kuwapa walengwa uelewa kuhusu Shirika la Viwango Tanzania (TBS), majukumu yake ikiwemo taratibu za uandaaji Viwango,Matumizi ya Viwango na faida zake.
Kuhusiana na viwango amesema ni nyaraka ambazo hutayarishwa kwa kuzingatia mfumo wa uwazi na ushirikishaji wa wadau mbalimbali wa sekta husika.
“Aidha,vinapokuwa vimekamilishwa na kupitishwa na mamlaka husika, ambayo kwa hapa nchini ni TBS, viwango huweka maainisho na misingi muhimu ya kuzingatia katika uzalishaji wa bidhaa, utoaji huduma katika maeneo mbalimbali ya jamii na utendaji katika sekta mbalimbali ikiwemo sanaa, utamaduni na maeneo ya urithi.
Amesema matakwa ya viwango yanazingatia kuwezesha kutolewa kwa bidhaa na huduma bora kwa jamii husika, hivyo kulinda afya, usalama na mazingira na hatimaye kuchangia katika uchumi endelevu wa taifa.
“Pamoja na kwamba viwango vyenyewe hutayarishwa kwa uwazi na ushirikishwaji, lakini pia huweka misingi ya uwazi katika maainisho yake. Aidha, maainisho yake huweza kutumiwa na taasisi mbalimbali za udhibiti kutengeneza kanuni zinazosimamia masuala mbalimbali katika jamii yahusuyo ubora, usalama, afya, ulinzi wa mazingira, biashara na hata uadilifu katika utendaji,”amesema.
Amesema ili kutimiza majukumu haya muhimu kwa umma wa Watanzania, na pia kwenda sanjari na mikakati mingine ya kitaifa, tumeamua kuendesha mafunzo haya kwa watumishi wa halmashauri zote nchini.
“Hivyo tutaendelea kutoa mafunzo ya aina hii kwa mikoa mingine kwa utaratibu huu. Tunaomba watumishi watambue umuhumu kwa kushiriki vyema wakati wote wa mafunzo haya ikiwa ni pamoja na usikivu, kuuliza maswali pamoja na kutoa maoni yao kuhusu mada mbalimbali zitakazowasilishwa,”amesema.
Credit – Fullshangwe Blog.