DAR ES SALAAM.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezindua muongozo wa matibabu nchini na orodha ya taifa ya dawa muhimu (STG/NEMLT) toleo la Sita katika hafla fupi ilifanyika jijini Dodoma.
Waziri Gwajima amesema muongozo huo ni nyenzo muhimu inayotumika kuhakikisha kuwa ubora unazingatiwa katika kutoa tiba kwa jamii.
“Muongozo huu umepitiwa ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kitabibu. Aidha, umezingatia mabadiliko ambayo yameainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na mashirika mengine ya kitaifa na kimataifa kulingana na tafiti mbalimbali”. Amesema Dkt. Gwajima.
Waziri Gwajima ameainisha mabadiliko muhimu katika toleo la sita ikiwa ni Pamoja na kutoa muongozo juu ya menejimenti ya matibabu ya ugonjwa wa Corona (Covid-19) ambayo yametolewa ufafanuzi katika sura ya magonjwa ya mlipuko (notifiable diseases). Pia imeandaliwa sura mpya ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema katika kuimarisha huduma za afya nchini, kuna dawa 101 zimeongezwa katika orodha mpya kutokana na mabadiliko ya matibabu kwa kuzingatia Ushahidi wa kisayansi. Baadhi ya dawa zimeongezwa kukidhi maboresho ya huduma za kibingwa kama kupandikiza figo.
Vilevile katika kuboresha huduma za afya ya msingi dawa zimeshushwa kutoka ngazi ya Hospitali ya wilaya hadi ngazi ya vituo vya afya ili kuboresha huduma za dharura za mama na mtoto(CeMONC) hususan huduma za upasuaji huku baadhi ya dawa zikiondolewa katika orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu kwa sababu ya usalama, ufanisi na ubora wa kutosha.
Kuhusu usugu wa vimelea dhidi ya dawa aina ya antibiotiki, Waziri Gwajima amesema unaweka katika mashaka makubwa ya kupoteza nguvu kazi kwa kusababisha vifo kutokana na kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyotibika yanayosababishwa na kutumia dawa hizo kiholela.
Waziri Gwajima amesisitiza kuwa muongozo huo umeorodhesha dawa kulingana na ngazi ya kutolea huduma pia umezingatia ushauri wa wataalamu katika uandishi wa dawa ambapo hivi sasa Daktari bingwa anaruhusiwa kuandika dawa zote zilizopo kwenye muongozo kulingana na eneo lake la kitaaluma bila kuzingatia ngazi anayofanyia kazi.
Mwisho, Waziri Gwajima amesema dawa muhimu zinatakiwa zipatikane kwa wakati wote katika vituo vya kutolea huduma hivyo amewaagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuzingatia orodha ya dawa muhimu katika ununuzi wa dawa nchini.