Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo (wa pili kushoto) akiweka saini kwenye kitabu cha wageni katika moja ya Taasisi zinazoshiriki Maonesho hayo.
Na: Mwandishi wetu, DAR.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 45 ya biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya maonesho Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake fupi kwenye maonesho hayo Waziri wa viwanda na biashara Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo utafanyika Julai 5, mwaka huu.
“Tunaomba Wananchi wajitokeze Kwa wingi ili kuja kumuunga mkono Rais na wao kuweza kupata fursa ya kutembelea Maonesho haya ya 45 ,na kama nilivyosema julai 5 kuanzia saa nane mchana mgeni rasmi atakuwa kwenye viwanja hivi..”amesema Prof. Mkumbo.
Amesema kuwa mandalizi ya maonesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Uchumi wa Viwanda Kwa Ajira na Biashara endelevu’ yamekamilika na kwamba washiriki 3002 wamethibitisha kushiriki huku nchi 7 za kigeni zikithibitisha kushiriki yakiwemo makampuni 76.
Akizungumzia ratiba za shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika maonesho hayo Prof. Mkumbo amesema kuwa kutakuwa na uzinduzi wa mfumo wa taarifa za biashara ambao utaongeza uwazi wa taratibu za biashara kimataifa ambapo utaongeza wigo wa taarifa za biashara, pia kutazinduliwa Duka la kimtandao kwa ushirikiano wa Tantrade na Shirika la posta. (Mobile Shop).
Sambamba na hilo Prof. Kitila ameongeza kuwa kutafanyika uzinduzi wa kutambua mabanda ya washiriki wa ndani ya uwanja Kwenye maonesho hayo ambapo kumeandaliwa ramani ya kuonesha maeneo yaliyopo mabanda ili wananchi waweze kujua mahali anapotaka kwenda kulingana na Banda husika analolihitaji.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuchukua taadhali za kujinga na wimbi la corona kwa kufuata miongozo mbalimbali ya wizara ya Afya huku akitaja viingilio kuwa ni 1000 kwa watoto na wakubwa 3000 ambapo kwa siku yenyewe ya sabasaba kiingilio kitakuwa 4000 kwa wakubwa na watoto 1000