MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewaagiza wamiliki wote wa vituo vya mafuta ya petroli nchini kuhakikisha wanachukua hatua stahiki zinazozingatia usalama wa afya, mali na mazingira wakati wote wa uendeshaji wa biashara hizo.
EWURA imetoa agizo hilo kutokana na ongezeko la matukio ya milipuko ya moto inayotokana na uhifadhi au uuzaji holela wa mafuta ya petroli kwa kutumia madumu au chupa jambo kinyume na tahadhari za usalama wa afya, mali na mazingira (HSE).
Taarifa iliyotolewa Septemba 16, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, imewasisitiza wafanyabiashara ya vituo vya mafuta nchini kutoruhusu uuzwaji wa mafuta katika vifaa visivyoruhusiwa kuchukulia au kubebea mafuta ya petroli kama vile madumu, chupa aina zote na vifaa vingine visivyoruhusiwa kisheria.
“Tunawahimiza wamiliki wa vituo vya mafuta kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha ya watu, mali, na mazingira wakati wa uendeshaji wa biashara zao na kuchukua tahadhari stahiki kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 27 ya Kanuni zinasimamia biashara ya vituo vya mafuta nchini”.
Pia, EWURA imebainisha kuwa, itaendelea kufanya ukaguzi wa kina kwenye vituo vya mafuta kote nchini ili kuhakikisha utekelezwaji wa kanuni hizo, na yeyote atakayekiuka hatua kali za kisheria ziatachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufungiwa vituo vyao.