DAR ES SALAAM.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla leo Juni 28 amepokea Mabasi 70 ya Mwendokasi kwaajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya Usafiri kwa Wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza wakati wa kupokea Mabasi hayo RC Makalla amesema anafurashwa kuona Mafanikio hayo yamepatikana ndani ya Siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo amesema upatikanaji wa Magari hayo utaenda kutatua kero za Wananchi.
Aidha RC Makalla amesema Serikali imejipanga kutatua changamoto ya Mafuriko Dar es salaam hususani eneo la Jangwani ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu wa kusimama kwa huduma za usafiri nyakati za mvua.
Changamoto nyingine ambazo RC Makalla amezipokea kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UDART na kuahidi kuzipatia ufumbuzi ni Kero ya Bodaboda kuingia kwenye Barabara na Magari binafsi za Mwendokasi na Wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwenye Barabara za Mwendokasi.