Home BUSINESS BASHE NA MPINA: MAENDELEO KWANZA, SIASA PEMBENI

BASHE NA MPINA: MAENDELEO KWANZA, SIASA PEMBENI

“Wananchi wa Kisesa tunaenda kuandika historia kubwa kwenye nchi yetu, tupo kwenye mkutano huu pamoja kwa ajili ya maendeleo. Waziri Hussein Bashe Unakaribishwa sana katika Jimbo langu la Kisesa,” amesema Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina.

Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo ameendelea na ziara yake mkoani Simiyu leo tarehe 13 Septemba 2024 ambapo asubuhi alitembelea mradi wa umwagiliaji wenye bwawa lenye ujazo wa cubic meter 2.7 milioni uliopo Kasoli, katika Halmashauri ya Shinyanga. Mradi wa umwagiliaji Kasoli ni sehemu ya mradi wa Nyida, ambao una thamani ya shilingi bilioni 8, ujenzi umefikia asilimia 60 na utakamilika mwezi Aprili 2025.

Adha, hekta 634 za mradi huo zinakadiriwa kuhudumia wakulima baada ya bwawa hilo kukamilika. Waziri Bashe ameelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha pia inajenga barabara kuelekea kwenye bwawa na kujenga ghala na ununuzi wa kinu cha kukobolea mpunga ili kurahisisha mahitaji ya wakulima.

Katika Mkutano wa hadhara na wananchi waliojitokeza kwenye uwanja wa mpira wa Mwandoya, kwenye Wilaya ya Meatu, Waziri Bashe alitoa shukrani kwa heshima aliyopatiwa na wananchi na wataalamu wa tiba ya asili wa Mkoa wa Simiyu ambao wamempatia jina la “Jifunika”, kwa maana kujifunika mabaya yoyote.



 

“Nitoe Salamu za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha nyingi kuinua tasnia ya Pamba na ameendelea kutoa pembejeo, matrekta na huduma za ugani kwa wakulima wa zao la Pamba,” amesema Waziri Bashe. Ameeleza kuwa kutakuwa na ujenzi wa mabwawa matatu (mawili katika jimbo la Kisesa) na moja katika Kijiji cha Mwagila.

Ameelekeza pia katika trekta 40 alizozigawa katika vituo viwili leo vya Mwanhuzi na Mwandoya, wakulima watoa we gharama za Shilingi 35,000 kulima mashamba yao, tofauti na gharama ambazo wamekuwa wakitozwa shilingi 50,000 hadi 60,000 kulima kabla ya kupatiwa matrekta leo hii.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Kihongosi amesema “tusikubali kuingiza siasa kwenye kilimo kwenye maisha ya wananchi wetu ambao wanatutegemea.“

Mkuu wa Mkoa amemuomba Waziri Bashe arejeshe kitalu cha mbegu mkoani Simiyu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here