Zana hizo zimekabidhiwa na Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo kufuatia ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora tarehe 11 Septemba 2024.
“Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuendelea kuwekeza kwa wakulima ili wazalishe mazao kwa tija. Na tutaendelea na mpango wa kuchimba mabwawa ili waanze pia kuvuna maji ya mvua na kuwa na Kilimo cha umwagiliaji,”amesema Mhe. Waziri Bashe.
Ameongeza kuwa ni vyema wakulima hao kutumia ipasavyo fursa na nyenzo hizo za kilimo na kupuuza baadhi ya wanasiasa.
“Serikali hii haiwezi kutoa dawa feki, mbegu feki na wanunuzi feki kwa wakulima. Siasa zinaleta uchochezi kwa wakulima zinaharibu maisha ya watu na hilo sitoruhusu huo mchezo kwenye Sekta ninayosimamia,”amesema Waziri Bashe.
Amefafanua zaidi kuwa “hatuwezi kuwa na Taifa linatukana watu, linatukana Serikali tunakaa kimya. Watu walikuwa na mateso walikopwa, pamba zilidoda. Miaka miwili tumetoa ruzuku ya mbolea bure na tutaendelea kufanya hivyo na tutaendelea kununua mazao.” Pia ameeleza nia ya wizara kuweka kituo cha ununuzi wa nafaka Wilayani Igunga.
Aidha, Mhe. Waziri Bashe ametumia fursa hiyo kueleza mipango ya Serikali ya kujenga mabwawa na miundombinu ya umwagiliaji ya kutosha Igunga kwa kuwa kitakwimu ni ya kwanza au ya pili, hivyo ni lazima kuwa na uzalishaji wa uhakika kwa kilimo cha umwagiliaji cha Pamba.