Na: Mwandishi wetu,DODOMA.
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dkt.Doroth Gwajima amelitaka Baraza la la Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NaCONGO) kufanya kazi kwa weledi,uadilifu na uzalendo pamoja na kuzingatia Sheria,kanuni, na miongozo iliyopo ili kukidhi matarajio ya waliowachagua.
Hayo ameyasema leo,Julai 10,2021 jijini Dodoma wakati akipokea taarifa na kuzindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyokuwa yakiserikali (NaCONGO),Waziri Gwajima amelitaka Baraza hilo kufanya kazi weledi,uadilifu na uzalendo.
“Nitoe wito kwa viongozi na Wajumbe kufanya kazi kwa weledi,uadilifu na uzalendo pamoja na kuzingatia Sheria,kanuni, na miongozo iliyopo ili kukidhi matarajio ya waliowachagua na Jamii ya watanzania kwa ujumla,”amesema
Waziri Gwajima amesema hana shaka na uongozi mpya kwani wataweza kutoa ratiba mapema baada ya miaka mitatu uchaguzi ufanyike lini.
“Mmesema tangu mwaka 2019 lilikuwa mfu sasa sijui tulikuwa tunafanyaje kazi,Baraza hili nimeliamini sina Shaka na weledi,haiba yenu na mtasema haraka lini uchaguzi ufanyike baada ya miaka mitatu,”amesema
Amesema Baraza hilo lilifanya uchaguzi mwaka 2016 ambapo mara baada ya hapo waliokuwa viongozi waligoma kufanya uchaguzi.
“Mimi nasema baraza hili liligoma sasa tuwaache ninyi tizameni mbele hao waliogoma mungu anawaona.Kutokufanyika kwa uchaguzi kunasababisha baadhi ya Vyombo vishindwe kufanya kazi,”amesema.
Amesema viongozi wa Kamati ya mpito wamefanya kazi nzuri kwani lilikuwa mambo yalikuwa ni mazito.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa kusimamia zoezi hili,Tunautambua umuhimu wenu hivyo tunawapongeza sana,”amesema.
Waziri Gwajima amemtaka Mwenyekiti wa Baraza hilo,Lilian Badi kusimamia mambo yaende vizuri huku akidai kwenye mambo ya fedha Mayuda huwa hawakosekani.
“Baraza hili ni zito simama kwenye nafasi yako kwenye pesa mayuda hawakosekani,”amesema
Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii,Dkt.John Jingu ameipongeza Kamati ya mpito kwa kusimamia vizuri uchaguzi.
“Nilikuwa na wasiwasi mwezi mmoja utatosha Leo tunathibitisha kweli umetosha ila watanzania wana matumaini makubwa nendeni mkasimamie Sheria na muwe waadilifu,”amesema.
Kwa upande wake,Mwenyekiti mpya wa NaCONGO,Lilian Badi amesema wanaahidi kufanya kazi kisayansi na kwa uadilifu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuwajibika ambapo amedai wamedhamiria kuona NaCONGO inarudi katika ubora wake.
Amesema watakuwa mabalozi wa msajili katika Wilaya kwa kuhakikisha NGO’s zinafuata taratibu na sheria katika kujiendesha.
Pia,amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ambapo wameomba kuonana na Rais ili waseme kile ambacho wanacho.
“Muda wa kuleta sintofahamu hatuna sisi tunataka kutoa Mchango kwa Taifa letu ila tunaomba (mgeni rasmi) Mwambie Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan tunampenda na mama yetu sio mgeni kwenye hii tasnia ya NGO’s,”amesema
Awali ,Mwenyekiti wa Kamati teule ambayo ilisimamia uchaguzi,Flaviana Charles amesema mara baada ya kuchaguliwa na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk.Doroth Gwajima June 7 mwaka huu walihakikisha uchaguzi unafanyika katika Mikoa 26 na Wilaya 139 kwa kushirikiana na Ofisi za Msajili.
Amesema katika chaguzi hizo walisimamia kanuni na vigezo ikiwemo mgombea kuwa mfanyakazi wa Shirika ambalo limekidhi vigezo vya NGO’s,kuwa raia wa Tanzania,kutokuwa na rekodi ya makosa ya jinai pamoja.
Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa baraza jipya kutengeneza ratiba mapema ya uchaguzi ujao kwani Tanzania ni kubwa,kutengeza kanuni mpya kwani za mwaka 2016 zimepitwa na wakati,kuwe na mfuko wa fedha,kutafuta wafadhili ili waweze kujiendesha,baadhi ya Mikoa iwe na wawakilishi wengi kwani ni mikubwa akitolea mfano Mkoa wa Dar es salaam.