DAR ES SALAAM
15/7/2021 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amekutana na Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) na ujumbe wake kwenye ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam na kupokea taarifa itokanayo na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wafamasia wa 27/05/2021 ambao Waziri huyo alikua Mgeni Rasmi.
Ujumbe huo ulimkabidhi Dkt. Gwajima taarifa ya maazimio tisa yaliyotokana na Mkutano huo kama alivyoagiza na maazimio hayo yaligusa maeneo ya kuimarisha zaidi maadili ya wanataalamu, kuongeza wataalamu wa kada husika, kuwezesha uwiano mzuri wa uwepo wa maduka ya dawa mijini na vijijini, kuboresha utaratibu wa utambuzi wa ngazi za wataalamu katika mfumo wa utumishi wa umma, kudhibiti makosa ya taarifa za dawa yanayopelekea makato makubwa ya fedha za bima ya afya, kuchochea kasi ya uzalishaji wa dawa kupitia viwanda vidogo vidogo, kuimarisha mfumo wa utoaji taarifa za madhara ya dawa (ADR), kuimarisha kasi ya usajili wa wanataalum na pia kuongeza kasi ya kudhibiti bidhaa zilizopitwa na wakati.
Dkt Gwajima amewapongeza wataalamu hao kwa kutekeleza maelekezo aliyotoa siku ya kufungua kikao chao na kuwa Wizara yake iko tayari kufanya kazi nao bega kwa bega pia na wengine wote wenye mapenzi mema ya kuleta mabadiliko ya haraka yaliyo chanya katika sekta ya afya.
“Mwelekeo wa Wizara ni kuwatambua wote mwenye mawazo chanya katika kuendeleza sekta hivyo wengine wote waliopewa maelekezo au bila maelekezo wajipambanue kuunganisha nguvu kwenye ujenzi wa sekta ya afya” Dkt. Gwajima.
Aidha, Dkt. Gwajima amemwambia Rais wa PST Bw.Fadhil Hezeniel yupo tayari kuwapa ushirikiano ili kuhakikisha taaluma ya famasia inafanya vizuri katika kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya nchini.