Home LOCAL DKT. BITEKO AWATAKA WAGOMBEA KUNADI SERA KISTAARABU

DKT. BITEKO AWATAKA WAGOMBEA KUNADI SERA KISTAARABU

Watanzania wameaswa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kwa kuchagua viongozi wanaofaa na watakaosaidia kuleta maendeleo nchini.

Hayo yamesemwa leo Agosti 31, 2024 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati aliposhiriki bonanza la michezo la Bunge lililokuwa na kauli mbiu inayosema shiriki uchaguzi kwa maendeleo ya Taifa.

‘‘Bonanza hili liwe chachu ya kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kuchagua viongozi wanaofaa kwa ajili ya kutuletea maendeleo katika Taifa hili. Viongozi watakao tuunganisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali bila kujali hali zao, dini zao, makabila yao wala vyama vyao vya siasa, bonanza hili litukumbushe kuwa tunaenda kuchagua viongozi wanaofaa kwenye utawala wa nchi hii, viongozi wa kitongoji au mwenyekiti wa kitongoji au kijiji hawa ni viongozi muhimu wanaokaa na watu wakati wote tusiwachukulie poa wakati wa uchaguzi huu, tuchague viongozi wenye uwezo,’’ amesema Dkt. Biteko.

Amefafanua ‘‘Uongozi utakao chaguliwa uwe kutokana na sifa na kampeni tusiruhusu kubaguana ama kutukanana badala ya kunadi sera zetu, bonanza hili litukumbushe pia kuwa baada ya uchaguzi maisha yanaendelea na maisha yataendelea tu kama tutachaguana kwa haki, upendo tukisisitiza umoja wa kitaifa na muungano wetu.’’

Vilevile, Dkt. Biteko ameipongeza Benki ya NMB kwa kuunga mkono juhudi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchangia kiasi cha fedha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bunge.

‘‘Nampongeza Spika wa Bunge kwa kufanya ubunifu wa kuwa na Bunge Bonanza ambalo limeleta mageuzi makubwa, kuonesha utu na kufanya wabunge wafurahie kazi yao na kuruhusu vipaji ili kuwa na Bunge Sports Club pamoja na Bunge Bonanza. Nawapongeza pia waheshimiwa wabunge wote kwa kushiriki michezo mbalimbali katika bonanza hili.’’ Amemaliza Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge na Rais wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameishukuru Benki ya NMB kwa kuwa wadau wa karibu wa Bunge na wabunge ambao wamekuwa wakishirikiana kwenye maeneo yao mbalimbali na kuwa bonanza hilo ni mojawapo tu, aidha kupitia ushirikino huo NMB imetoa mchango wao maalum kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bunge.

‘‘Shule hii inajengwa kwa kuwa Bunge lilishajenga Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge na sisi tunatambua kwamba watoto wa kike lazima wapate elimu iliyo bora na watoto wetu wa kiume pia wapate elimu iliyo bora na hivyo tumejenga shule bora ya wasichana na tunajenga ya wavulana na hiyo hii itakuwa imeweka uwiano sawa kuwa Bunge tunathamiani watoto wa kike na wakiume.’’ Amesema Dkt. Tulia.

Pia, ametoa wito kwa wadau wengine kuwa kuendelea kutoa michango yao ili ujenzi wa shule hiyo ukamilike kwa wakati.

Naye, Mwakilishi wa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Yahya Rashid Abdulla amesema kuwa Baraza la wawakilishi litaendeleza ushirikiano uliopo katika kati ya mabunge hayo mawili.

Mwenyekiti wa Bonanza la Bunge Mhe. Festo Sanga amesema ‘‘Spika alielekeza Bunge lifanyekazi kama taasisi hivyo ni muhimu kuwa na ushirikiano na taasisi zingine na leo katika bonanza hili tumeshirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Benki ya NMB. ’’ Amesema Mhe. Sanga.

Vilevile, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw Juma Kimori amesema kuwa Bunge limekuwa likishirikiana na NMB kwa masuala ya kifedha na kuwa wanawashukuru wabunge kwa kuendelea kutumia huduma zao pamoja na kushirikiana na benki hiyo katika majimbo yao.

‘‘Katika programu zetu za kurudisha kwa jamii tumekuwa tukishirikiana katika elimu, afya na masuala mbalimbali, NMB itaendelea kushirikiana na nyie katika kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali, NMB imejikita katika kuleta suluhisho kwa jamii yetu na sasa tuna programu ya kuhakikisha tunafika katika kila kijiji Tanzania mfano mikopo mshiko fasta ni mkopo unaomlenga mwananchi ambao hauna masharti kama mikopo mingine. ’’ Amesisitiza.

Awali Dkt. Biteko ameshiriki bonanza la Bunge katika matembezi kutoka Chuo cha Mipango hadi Viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini na baada kutoa zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali.

Previous articleNIC YATAMBULISHA BIDHAA MPYA ‘BIMA YA MAISHA’ KWA WAKUU WA TAASISI ZA SERIKALI
Next articleMATI SUPER BRANDS YASHIRIKI MANYARA DAFTARI DAY JOGGING

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here