Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha inawawezesha wakulima wadogo na wa kati kupata mikopo itakayowawezesha kuzalisha kwa tija mazao yao, lakini pia kuyaongezea thamani yaweze kuuzwa ndani na nje ya nchi.
TCB katika mkakati wake wa kupanua wigo kwenye sekta ya kilimo biashara, imejikita kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili kuweza kutoa mikopo na kuongeza thamani kwenye mnyororo wa sekta ya kilimo.
Haya yameelezwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mikopo kutoka Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Bwana Daniel Mbotto katika kikao cha pamoja cha kujengeana uwezo kwenye utoaji wa mikopo kwa sekta ya kilimo kati ya TCB na wataalmu waelekezi Aceli Africa na AFC GOPA.
Mbotto ameeleza kuwa katika mkakati wa kukuza kilimo nchini, na kwa kuzingatia mtandao mpana wa matawi 82 ya TCB, itahakikisha wafanyakazi wana uelewa wa kutosha kwenye utoaji wa mikopo ili kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.
“Tutaendelea kutoa mikopo huku tukiongeza ubunifu kupitia uzoefu ili kuweza kuwafikia na kuwasaidia wakulima hao kwa kutoa suluhisho na kukuza mitaji yao,” amesema Mbotto.
Aidha, Mbotto amebainisha kuwa mwitikio wa wakulima hao kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo ni kubwa, hasa kwenye zao la muhogo huko Kibondo, ambako wakulima wamenufaika na uzalishaji wa zao hilo hasa kwenye msimu wa 21 na 22 na hivi sasa wanaingia kwenye msimu wa 23 na 24.
“Kikubwa ni kuhakikisha TCB inaisaidia serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi, na kuwafikia wakulima na kuwasaidia wao na familia zao. Pia, inaongeza tija, mapato, na mitaji yao ambayo itawasaidia kufungua biashara nyingine na kuendelea zaidi.”
Katika jitihada zote hizo ambazo zimekuwa zikifanyika kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wakulima wanakuwa na tija, kwenye zao hilo la muhogo kuna baadhi ya wakulima wamekwishaanza kuweka viwanda vidogo vya kuliongezea thamani zao hilo na hata kuweza kuuza kwenye nchi za Ulaya na Marekani.