Home BUSINESS TANZANIA KUSHIRIKIANA NA CUBA UTAFITI WA MIMEA TIBA-MAJALIWA

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA CUBA UTAFITI WA MIMEA TIBA-MAJALIWA

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema ni muhimu kwa Tanzania na Cuba kuimarisha uhusiano katika eneo la utafiti na matumizi ya mimea tiba kwa ajili ya kutengeneza dawa za magonjwa mbalimbali ya binadamu nchini.

Mheshimiwa Majaliwa aliyasema hayo Agosti 13, 2024 baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Cardenas kwa kutumia mimea tiba kilichopo katika Jimbo la Matanzas, akiwa katika ziara maalum nchini Cuba.

Alisema ipo haja kwa Watafiti wa mimea tiba kutoka nchini Cuba kuja Tanzania na kufanya utafiti wa mimea dawa inayofanana na ile wanayotumia nchini kwao ili kuona kama itafaa kutengeneza dawa.

“ Kama leo Cuba wanasema ugonjwa wa UKIMWI umepungua kwa zaidi ya asilimia 98, haya ni mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa kutumia dawa ambazo wao wenyewe wanazitengeneza. Wacuba wanasema tatizo la magonjwa kama ya moyo, saratani na kisukari yamepungua kwa kiasi kikubwa, hayo ni mafanikio makubwa”. Alisema Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema kuwa “Tanzania tunayo sera ya matumizi ya dawa za asili ambazo zinatambulika na Wizara ya Afya na wale wote wanaojishughulisha na tiba asili wamesajiliwa na Serikali, hivyo uko umuhimu wa kuendeleza mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Cuba kwenye sekta ya afya ili kuruhusu aina hizi za dawa kutumika nchini. Wizara ya Afya ipanue wigo wa mazungumzo kwa ajili ya utekelezaji.”

Alisema Cuba ina viwanda zaidi ya 72 vinavyotumia malighafi ya mimea tiba na dawa hizo zinatambulika na Serikali na zimeisaidia nchi hiyo kupunguza bajeti ya kuagiza kutoka nje ya nchi kwa asilimia 60.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Majaliwa alifuatana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Balozi Humphrey Polepole.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here