Home BUSINESS MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZA NA UJUMBE JUKWAA LA UCHUMI DUNIANI (WEF)...

MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZA NA UJUMBE JUKWAA LA UCHUMI DUNIANI (WEF) DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Ujumbe wa Sekretariet ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) wakiongozwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki Bi. Clemence Schmid, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Agosti 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 15 Agosti 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Sekretariet ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) wakiongozwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki Bi. Clemence Schmid, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema serikali imedhamiria kushirikiana na wadau, sekta binafsi pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kupambana na tatizo la taka za plastiki nchini. Amesema uzoefu unaonesha kwamba ushirikiano ni njia bora zaidi itakayowezesha kukabiliana na tatizo hilo kwani yapo maeneo ambayo taka za plastiki hutupwa na kufika katika mataifa mengine hususani kwa njia ya bahari.

Amewakaribisha Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) kupitia Ushirikiano wa Kimataifa katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki kushirikiana na Tanzania katika mbinu mbalimbali za kukabiliana na uchafuzi wa taka za palstiki kama vile kuwajengea uwezo wataalamu, kuwezesha teknolojia na vifaa vya kisasa vya urejerezaji wa taka za plastiki pamoja na ufadhili wa kifedha katika miradi ya kukabiliana na uchafuzi wa taka za plastiki.

Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na taka za plastiki kama vile kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na utoaji elimu ya kuhamasisha wananchi kubadili tabia ya utupaji taka za plastiki ovyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) Bi. Clemence Schmid ameipongeza serikali ya Tanzania kwa jitihada na nia ya dhati ya kupambana na taka za plastiki.

Amesema ujumbe wa Sekretarieti ya Jukwaa la Uchumi Duniani umejionea dhamira ya dhati ya Tanzania katika kutoa kipaumbele cha juu kuzuia uchafuzi wa mazingira husasani wa taka za plastiki.

Amesema Jukwaa hilo linalenga kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania kwa lengo kuu la kuondoa taka za plastiki ambapo kupitia ushirikiano huo Tanzania inaweka mazingira rafiki ya kuongeza kushirikisha wadau wa kitaifa na kimataifa katika kuiondoa nchi kwenya adha ya taka za plastiki.

Ametaja vipaumbele katika ushirikiano huo ni pamoja na kutambua changamoto zilizopo, kuwaunganisha wadau pamoja na kutambua namna ya kutumia rasilimali fedha na uwekezaji katika kuandaa miundombinu rafiki ya kutumia vema taka za plastiki kiuchumi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Sekretariet ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) wakiongozwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki Bi. Clemence Schmid (mwenye gauni jeupe) pamoja na ujumbe wa Tanzania mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Agosti 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Ujumbe wa Sekretariet ya Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) wakiongozwa na Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano katika Usimamizi na Menejimenti ya Taka za Plastiki Bi. Clemence Schmid (mwenye gauni jeupe) mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 15 Agosti 2024.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
15 Agosti 2024
Dodoma.

Previous articleWAZIRI JAFO ATAKA KILA MKOA KUANZISHA VIWANDA
Next articleRAIS SAMIA AWASILI HARARE NCHINI ZIMBABWE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here