Home LOCAL MWENYEKITI NA KATIBU WA TUME YA UTUMISHI WALIMU WASHIRIKI UZINDUZI RASMI WA...

MWENYEKITI NA KATIBU WA TUME YA UTUMISHI WALIMU WASHIRIKI UZINDUZI RASMI WA UTOAJI CHANJO YA UVIKO-19 MKOANI DODOMA

DODOMA

Mwenyekekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Prof. Willy Lazaro Komba na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Mbena Nkwama, wameshiriki katika Uzinduzi wa Utoaji Rasmi wa Chanzo ya UVIKO-19 uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma siku ya Jumanne Agosti 03, 2021 ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mkoa, Wilaya, Madhehebu mbalimbali, Vyama vya Siasa, Taasisi, Jumuiya na Wananchi wa Mkoa wa Dodoma na viunga vyake. 


Akizindua utoaji chanjo huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka amewataka Watanzania kuacha kuwa matomaso wa kwenye vitabu vya dini ili kuamini suala la chanjo ya UVIKO-19 na badala yake wajitokeze kuchanja wakati huu baada ya chanjo kufika katika maeneo yetu kwani Serikali imeona uhitaji wa na umuhimu wa chanjo hii muhimu badala ya kusubiri hali zikiwa mbaya na upatikanaji wake kuwa wa shida kutokana na mlundikano na misururu mikubwa ya wahitaji baada ya kuamini chanjo hiyo inasaidia. 


Pamoja na hilo Mhe. Mtaka amelielekeza Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kuhakikishia wanasimamia utekelezaji wa abiria kukaa ‘level seat’ kwenye magari wakati wafanyabiashara kwenye masoko wakitoa huduma wakiwa wamevaa barakoa na menejimenti za masoko zikihakikisha kuwa kuna maji tiririka ya wananchi kunawa huku akiwaomba wamiliki wa vyombo vya usafiri kusaidia kama kuna uwezekano wa kupata barakoa basi wafanye hivyo ikiwa ni pamoja na kuepuka kubananisha watu katika maeneo ya biashara. 


“Katika mazungumzo yangu na Jeshi la Polisi nimeelekeza pia tusiruhusu mishikaki kwa maana ya kupandisha abiria zaidi ya mmoja katika pikipiki moja na matumizi ya kofia za kujilinda na usalama katika pikipiki usiruhusiwe kwa zaidi ya mtu mmoja katika kipindi hiki cha ugonjwa, na badala yake kofia hizo zivaliwe na madereva wenyewe wa pikipiki walau kuwa tumesaidia sehemu moja ya kuepusha umbukizaji na usambaaji wa ugonjwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.” Amesema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma 


Mkuu wa Mkoa Mtaka kabla ya kumkaribisha Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, Prof. Willy Komba ili kutoa neno kwa wananchi walioshiriki uzinduzi huo amekiri yeye binafsi kupoteza ndugu takribani 20 kwa janga la UVIKO-19 na wengine kupona kwa msaada wa kupatiwa hewa ya Oksijeni hivyo kutoa shime ya kujitokeza kuchanja kabla ya kuanza kuomba misaada ya kupata huduma hiyo ya chanjo hali zitakapobadilika na kuwa mbaya zaidi. 


Nae Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwl. Paulina Nkwama kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume, Prof. Willy Komba na Uongozi wa Tume, akitoa neno kwa wananchi walioshiriki uzinduzi huo amesema anaushukuru Uongozi wa Mkoa na Serikali kwa kuleta chanjo hizo na kuahidi kuendelea kuhamasisha walimu kujitokeza kupata chanjo hiyo kwa hiari kwani walimu ni kundi kubwa katika utumishi wa umma na wanategemewa na kila fani katika Taifa lolote duniani hivyo ni vema kujitokeza na kupata chanjo hiyo ili kulinda afya kwa hiari na kuendelea kutoa elimu kwa kada zote zinazowategemea kwa maendeleo ya Taifa na ukuaji wa uchumi. 


Takwimu za awali zilionyesha zaidi ya watu 1,000 walishajitokeza na kuomba kuchanjwa mara chanjo hiyo itakapofika mkoani hapa na hii imedhihirika katika uzinduzi ambapo viongozi na wananchi waliojitokeza ni zaidi ya idadi hiyo na hivyo kuashiria mapokeo chanya ya chanjo hii ya UVIKO-19. 


Mwisho.

Previous articleKARIBU USOME HABARI MAGAZETI YA LEO J.TANO AGOSTI 4-2021
Next articlePHILIP AWAFUNDA WANAMITINDO KUACHA UTEGEMEZI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here