Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi (kulia) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Viongozi wa Idara za Serikali na Mahakama wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati akikagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ikungi.
SERIKALI kuanza ujenzi wa Mahakama Kuu katika mikoa tisa nchini iliyobaki ukiwemo Mkoa wa Singida ili kuondoa tatizo la wananchi kusafari kwenda mikoa ya jirani kwa ajili ya kupata huduma za Kimahama.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi wilayani Ikungi mkoani hapa katika ziara yake ya kukagua Mahakama za wilaya na za Mwanzo pamoja na kuzungumza na wadau wa masuala ya Sheria.
Kabudi alisema alisema mpango wa ujenzi wa mahakama hizo utaenda pamoja na ujenzi wa mahakama za wilaya hasa kwenye wilaya ambazo hazina mahakama.
” Wilaya ya Ikungi nayo itaingizwa kwenye mpango wa ujenzi wa mahakama ya wilaya kwa sababu mpaka sasa haina mahakama ya wilaya ambapo wananchi wanafuata huduma za kimahakama mjini Singida,”. alisema Profesa Kabudi.
Aidha Waziri Kabudi amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Ikungi kwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya wilaya na kusema jambo hilo ni nzuri na linapaswa kuigwa na wilaya nyingine.
Akizungumzia kuhusu ukarabati wa mahakama za mwanzo nchini, Profesa Kabudi alisema utafanyika kwa awamu na kipaumbele kitatolewa kwenye Mahakama za Mwanzo ambazo zinahudumia idadi kubwa ya wananchi.