Home LOCAL MALIKI HASHIMU  ARUHUSIWA KWENDA NYUMBANI

MALIKI HASHIMU  ARUHUSIWA KWENDA NYUMBANI

WAZAZI WAMSHUKURU MHE. RAIS, WATOA HUDUMA, VYOMBO VYA HABARI NA WATANZANIA WOTE

Mtoto Maliki Hashimu, mkazi wa Goba Jijini Dar es Salaam, aliyekuwa akitibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na majeraha makubwa aliyopata baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni kilichotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti na kusababisha ashindwe kupumua, kuongea, kupata maumivu na kupoteza damu nyingi, leo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya madaktari kujiridhisha na hali yake.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya kitabibu ya mtoto huyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhavile amesema, watalaam wa hospitali wamejiridhisha kulingana na huduma alizopata mtoto huyo tangu alipopokelewa Julai 15 mwaka huu kuwa sasa yupo salama na ataenda nyumbani ili kuendelea na shule na maisha yake ya kawaida huku hospitali ikiahidi kufuatilia kwa karibu maendeleo yake.

Kwa upande wa wazazi, Baba wa mtoto huyo Bw. Hashim Kitumbi kipekee amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa gharama za matibabu ya mtoto huyo, watoa huduma wote wa Hospitali walioshiriki kumuhudumia mpaka hatua aliyofikia leo kuruhusiwa, jamii ya watanzania walioguswa na tukio hilo pamoja na vyombo vya habari vilivyofuatilia kwa karibu jambo hilo.

Naye Daktari Bingwa wa Tiba na Magonjwa ya Dharura, Dkt. Juma Mfinanga amesema mara tu baada ya mtoto huyo kupokelewa akiwa na hali mbaya kutokana na majeraha aliyopata walihakikisha anapata huduma ya kwanza ya kurejesha hali ya upumuaji, kupata damu na badaye kuita timu husika ya wabobezi wa upasuaji wa shingo, pua, koo na masikio.

Dkt. Aslam Nkya Mbobezi wa Upasuaji wa Shingo amesema kwa kushirikiana na timu ya watalaam waliweza kumfanyia upasuaji mkubwa mtoto huyo ambao ulichukua muda wa saa nne ili kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi yaliyopata changamoto kwenye shingo na kutibu jeraha la nyuma ya shingo.

Dkt. Nkya amesema jeraha la mbele ya shingo, liliharibu tezi la mbele liitwalo (thyroid gland) kwa kulikata katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi, kupata maumivu makali kutokana na jeraha alilokatwa mbele ya shingo sehemu iitwayo (trachea) ambako hewa inayotoka kwenye mapafu hupita ili iweze kwenda kwenye sanduku la sauti kumuwezesha kuhema na kuongea kwa mantiki.

Naye Dkt. Namala Mkopi Daktari Bingwa Mbobezi wa Watoto wanaohitaji Uangalizi Maalum (PICU) amesema mara ya baada ya kufanyiwa upasuaji wamemhudumia katika eneo hilo wakishirikiana na watoa huduma mbalimbali hasa wauguzi, watalaam wa lishe na fiziotherapia ili kuhakikisha mtoto anapata huduma zote stahiki hivyo kutoka kwenye hatari ya kupoteza maisha.

Previous articleUDOM WAFANIKIWA KUBUNI MIFUMO YA TEHAMA
Next articleRAIS SAMIA AZINDUA KIWANDA CHA SUKARI CHA MKULAZI MOROGORO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here