Home BUSINESS HALMASHAURI ZASHAURIWA KUINGIA UBIA NA TFS KUANZISHA MASHAMBA YA MITI.

HALMASHAURI ZASHAURIWA KUINGIA UBIA NA TFS KUANZISHA MASHAMBA YA MITI.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS (Aliyevaa Shati jeupe), Mhandisi Enock Nyanda akiongea na maafisa wa TFS baada ya kutembelea Kitalu Kikuu cha Miche ya Miti kinachosimamia na TFS katika manispaa ya Musoma

BUTIAMA.

HALMASHAURI za wilaya, miji, manispaa na majiji zimeshauriwa kuingia ubia na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kuanzisha mashamba ya miti ya biashara.

Ushauri huo ulitolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS,  Enock Nyanda akisema wakifanya hivyo wataongeza vyanzo vya mapato kwani baada ya kuvuna na kuuza miti mapato yatagawanywa kwa wabia.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza,  imechangamkia fursa hiyo kwa kuingia ubia na TFS ambapo imetoa eneo kwa ajili ya kupanda miti na TFS ikitoa miche na utaalamu.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Dkt Siima Bakangesa alisema  ili kuwa sehemu ya wadau wa kukuza utalii nchini, wametambua Msitu wa Asili wa Kyarano, wilayani Butiama ambao ulitangazwa na hayati baba wa Taifa, Julius Kambaragr Nyerere kuwa msitu wa hifadhi.

“Tumeuchukua na kwa kushirikiana na wadau tunatiendeleza shughuli za uhifadhi za ufugaji wa nyuki na uoteshaji wa miche ya miti kwenye vitalu,” alisema Dkt Bakangesa.

Alisema hatua hizo zinatekelezwa kwa kuzingatia kuwa ili Wizara ya Maliasilo na Utalii imejiwekea malengo ya kuwapokea watalii Milioni Tano, kutembelea vivutio mbalimbali na kwamba ili hayo yatimie kunahitajika vivutio vingi vya utalii katika nyanja tofauti  ikiwamo ufugaji wa nyuki na misitu ya asili.

Alisema licha ya utalii, hatua hiyo inalenga kuhifadhi ndoto ya hayati baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere za  kuhifadhi misitu  ya asili na kufuga Nyuki.

Afisa wa TFS, Ayubu Moga alisema katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 waligawa miche zaidi ya 330,000 kwa Taasisi za Umma, Taasisi Binafsi na kwa watu binafsi kwenye wilaya zote mkoani Mara.

Alisema kuwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 wanatarajia kusambaza miche milioni Moja mkoani humo ikiwamo michr ya miti ya matunda,mbao,kivuli, asili na itatolewa bure kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira.

Hayo yalielezwa baada ya ujumbe huo wa TFS  kufanya ziara ya kukagua shughuli zinazotekelezwa mkoani Mara.

Mwisho.

Previous articleVIONGOZI WA ACT-WAZALENDO WAWATEMBELEA WAKULIMA WA KARAFUU ZANZIBAR
Next articleTANZANIA YAINGIA MAKUBALIANO KUANZISHWA TAASISI YA UDHIBITI DAWA UMOJA WA AFRIKA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here