Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Tanzania imepata fursa ya kuwa Mwenyeji wa Kongamano la Pili la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN ),Kanda ya Afrika kuhusu utalii wa vyakula vya asili litakalofanyika mwaka 2025.
Ameyasema hayo leo jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe katika Kongamano la kwanza la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism ) kuhusu Utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Africa.
Amesema ni fursa ya kukuza mnyororo mzima wa thamani katika utalii hasa Utalii wa vyakula na itawagusa wadau wengi wakiwemo wakulima, wafugaji ,wavuvi, wazalishaji wa nafaka,wachakataji mafuta n.k
Ameongeza kuwa Kongamano hilo litaambatana na mashindano mbalimbali kwa ajili ya ubunifu ambapo wenye vyuo na wataalamu wengine watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka nchi nyingine za Afrika na duniani kwa ujumla.