Na: WMJJWM-Dodoma
Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa imeridhika na utekelezaji wa Programu hiyo kwa Wizara ya Nishati na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kupitia Sheria, Sera na Programu zao zilizolenga kuleta Kizazi chenye Usawa nchini.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yao mkoani Dodoma kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo Julai 12, 2024, Nangi Massawe amesema Taasisi hizo zimeonesha dhahiri katika kuhakikisha Kizazi chenye Usawa kinafikiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Ameongeza Wizara ya Nishati imekuwa ikihakikisha upatikanaji wa Umeme na Nishati safi ya kupikia ambazo zimekuwa chachu katika kumpunguzia adha mwanamke ya kupata Nishati safi ya kupikia na Nishati ya umeme katika maeneo mbalimbali.
“Sisi kama Kamati tunazipongeza hizi Taasisi na Taasisi mbalimbali ambazo zimeonesha jitahidi na nia ya kuunga mkono ahadi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na Kizazi chenye Usawa nchini” amesisitiza Nangi
Akizungumza wakati Kamati hiyo ilipotembelea Wizara ya Nishati Katibu Mkuu wa Wizara ya hiyo Mhandisi Felchesmi Mramba Wizara inatambua umuhimu wa kutekeleza programu hiyo ili kuleta usawa wa kijinsia katika utendaji na kuwainua wanawake katika nyanja zote za kijamii na Kiuchumi.
Amesema uwepo wa Nishati safi ya kupikia inapunguza athari za kupata magonjwa yanayosababishwa na kuvuta moshi wa kupikia kwa Wanawake.
“Tunafikiri sekta ya Nishati kuanzia Wizara na Taasisi zake tumejitahidi kutoa kipaumbele cha kutosha kwa masuala ya Jinsia yanayowagusa Sana Wanawake na watoto” ameeleza Mhandisi Mramba
“Tuchukulie mfano umeme unapokwenda Vijijini watoto wa kike wanapata muda zaidi wa kusoma kwa sababu ya tamaduni na Mila zetu inatakuwa watoto wa kike wanatumia muda zaidi wakirudi shule wanatafuta kuni lakini angalau akiwa amefanya vitu vyote kuna mwanga anaweza akakaa akajisomea” amesisitiza Mhandisi Mramba
Amesisitiza Wizara inaendelea kuunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia jambo ambalo linalenga kumpunguzia gharama mwanamke na kumpa muda mrefu wa kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
“Kwa programu hii hatuna budi kusema Rais Samia ndio kinara na hatupaswi kumuangusha wala kukwamisha jitihada zake za kutaka kumkwamua mwanamke na Mtoto wa kike kwa kuhakikisha Nishati ya umeme na nishati safi ya kupikia inawafikia” ameeleza Mhandisi Mramba
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Eliakim Maswi Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa Umma (PPRA) ameeleza Taasisi hiyo inatekeleza Programu hiyo ya kizazi chenye usawa na kwa Mwaka 2023 wameweza kusajili vikundi maalum 424 wakiwemo wanawake na pia katika mwaka huo wameweza kuhakikisha kwamba Makundi hayo maalum yamepata tenda zenye thamani ya bilioni 5.3 ambayo kwao ni kitu kikubwa sana katika kusimamia Usawa wa kijinsia.
Kamati hiyo ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu hiyo ilianza ziara yake mkoani Dodoma Julai 9, 2024 na imetembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi la jiji la Dodoma, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Wajasiriamali, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Nishati, Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa Umma, Vituo vya Malezi na Makuzi kwa Watoto na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na Dodoma.