Na: Mwandishi wetu, DAR
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),imewataka watanzania kuacha kutumia Dawa kiholela pale wanapojisikia kuumwa kutokana na madhara watakayoweza kuyapata kwa kukosa maelekezo sahihi kutoka kwa mtaalamu wa Afya baada ya kupata vipimo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Adam Fimbo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Aidha Mkurugenzi huyo ameelezea umuhimu wa wananchi alisema ni muhimu kabla ya mtu kutumia dawa kufuata ushauri wa daktari.
“Utumiaji holela wa Dawa bila kufuata ushauri wa kitaalamu hupelekea madhara anayoweza kumpata mtumiaji kutokana na kukosa Maelekezo ya Daktari hii imekuwa changamoto katika jamii” amesema Fimbo.
“Kazi yetu kubwa ni kuzikamata na matukio kama haya yapo na endapo tukibaini tunawakamata tunafanya ukaguzi kwa kushirikisha Jna jeshi la Polisi,” ameongeza.
Katika hatua nyinge amezungumzia tatizo la kuzagaa kwa Dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo zimekuwa zikitumika kiholela na kuleta athari kwa watumiaji ambapo amesema kuwa Mamlaka hiyo imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na tatizo hilo sambamba na kutoa elimu kwa jamii ya watanzania na wananchi wote kwa ujumla juu ya madhara ya Dawa hizo.
“Kuna matukio mengi ya watu kupoteza maisha na wengine kupata shinikizo la damu kuzidi kuongezeka kwa kasi, hivyo tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii nzima kuacha kutumia Dawa hizi kiholela kwa sababu zinasababisha vifo visivyotarajiwa na kuelimisha jamii matumizi sahihi ya kutumia“alisema.
MWISHO.