Home BUSINESS WIKI YA UTUMISHI WA UMMA, BRELA YAWANOA WANAFUNZI CHUO KIKUU TUMAINI DAR...

WIKI YA UTUMISHI WA UMMA, BRELA YAWANOA WANAFUNZI CHUO KIKUU TUMAINI DAR (DarTu)

DAR ES SALAAM 

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es salaam (DarTu) wameshauriwa kufuata sheria za usajili wa majina ya biashara, kampuni na huduma zingine za kibiashara zinazotolewa na Taasisi ya BRELA ili kuondoa usumbufu pale watakapoanzisha biashara au kampuni zao mara baada ya kuhitimu mafunzo Chuoni hapo.

Wito huo umetolewa na maafisa wa BRELA Juni 21, 2024 wakati wakitoa mafunzo maalumu ya usajili wa Biashara, Majina ya Biashara, Kampuni pamoja na Hataza ili kulinda kazi na bunifu mbalimbali zinazofanywa na wafanyabiashara ama wajasiriamali nchini.

Wanafunzi hao wametakiwa pia kusoma na kutafuta taarifa sahihi kuhusu mifumo ya usajili wa makampuni na leseni za biashara zinazotolewa na Taasisi ya BRELA na hivyo kuacha imani potofu zinazodai kuwa kumekuwa na mlolongo mrefu wakati wa kusajili majina ya biashara pamoja kampuni.

“Kwa sasa ninyi ni wanafunzi, wengine wakitoka hapo wanaweza kuanzisha biashara na utakapokuwa mfanyabiashara hakikisheni mnasimamia sheria za BRELA katika ufanyaji Biashara, kwa sasa mfumo wa ORS unaendelea kufanyiwa maboresho ambayo yatamsaidia mfanyabiashara na wanaotarajia kusajili majina ya biashara kuondokana na changamoto wanazokutana nazo wakati wa kujisajili” – Bi. Neema Kitala, Kaimu Mkuu Sehemu ya Hataza kutoka BRELA

Awali, Mkuu wa Chuo cha Tumaini Dar es salaam (DarTu) Profesa Burton LM Mwamila aliipongeza BRELA kwa kutoa elimu kwenye makundi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuhusu masuala ya usajili wa biashara, majina ya biashara pamoja na huduma zingine huku akiahidi ushirikiano zaidi hasa katika nyanja ya ubunifu na ujasiriamali.

“Ni muhimu wanafunzi wakafahamu sheria na taratibu za usajili pamoja na uanzishaji wa biashara ili kuondoa changamoto zitakazojitokeza pindi watakapoanzisha biashara au kampuni zao, tumeanzisha programu ya kuwasaidia wanafunzi kuchunguza matatizo kwenye jamii na kuyatengenezea mawazo ya kibiashara ambayo yatashindanishwa ili kuboreshwa katika mpango biashara kutokana na tatizo halisi la jamii” alisema Profesa Mwamila.

Aidha, Profesa Mwamila amebainisha kuwa washindi watakaopatikana kutokana na ushindani wa mawazo bunifu hayo watawekwa kwenye kituo hatamizi chuoni hapo ambako watapata ushauri wa namna ya kuendeleza biashara zao ikiwa ni pamoja na kuandaliwa semina mbalimbali namna ya kushughulikia biashara.

Miongoni mwa mambo waliyojifunza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es salaam (DarTu) hii leo ni pamoja na Sheria ya Majina ya Biashara, Faida za Kusajili jina la Biashara, Njia Bora ya kupata Leseni ya biashara kutoka BRELA (Leseni A) ambayo ina hadhi ya Kitaifa na Kimataifa.

Katika wasilisho lake kwa wanafunzi kuhusu faida ambazo mtu anaweza kuzipata kwa kusajili jina la biashara, mwakilishi kutoka BRELA kitengo cha usajili majina ya biashara Bw. Yusuph Mwakasyuka amezitaja miongozi mwa faida ni pamoja na kuitangaza na kupata fursa ya kujulikana na taasisi za kifedha ambazo zitamsaidia mfanyabiashara kupanua wigo wa biashara na kuvutia wawekezaji katika biashara.

Mafunzo maalumu kuhusu usajili wa biashara yametolewa kwa wanafunzi zaidi ya 500 kutoka Chuo cha Tumaini Dar es salaam ambao wanasomea kozi mbalimbali ikiwemo sharia, uandishi wa habari pamoja na wale wanaosema masuala ya ubunifu na ujasiriamali.

Previous articleMAJALIWA: TUTAYAENZI MEMA YOTE YALIYOFANYWA NA NZUNDA
Next articleJKT YATOA WITO VIJANA AMBAO HAWAKURIPOTI MAFUNZO YA LAZIMA KURIPOTI HARAKA MAKAMBINI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here