Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Mh. Jacobs Mwambegele akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuhusu uboreshaji wa Daftari la Wapiga kura , Sheria na Kanuni zake ambapo uzinduzi unatarajiwa kufanyika Julai Mosi mwaka huu mkoani Kigoma.
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari kalutoka vyombo mbalimbali katika mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Milimani City jijini Dar es salaam.
DAR ES SALAAM
Tume Huru ya Uchaguzi imetangaza siku ya rasmi ya Uzinduzi wa uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura nchini linalotarajiwa kuzinduliwa Julai 1,2024 mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa mkutano wa Tume huru ya taifa ya Uchaguzi (INEC) na waandishi wa habari uliofanyika leo Juni 13,2024 Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jacobs Mwambegele amesema Mgeni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na kwamba maandalizi yote kuelekea uboreshaji wa Daftari hilo yamekamilika.
“Siku ya uzinduzi huo ndio siku rasmi ya kuanza kwa zoezi hilo kuanza kwa mkoa wa Kigoma kisha mikoa mingine ya Katavi na Tabora na kufuatiwa na Kagera na Geita” amesema Jaji Mwambegele.
Aidha, meongeza kuwa uboreshaji wa awamu ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 ambapo zoezi litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo huku zoezi likitarajiwa kukamilika Machi, 2025.
Amesema uboreshaji huo utatumia teknolojia ya BVR Kits katika uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini.
“Maandalizi yote ya uzinduzi huu yamekamilika, nitoe wito kwa wananchi kujitokeza kushiriki katika kuboresha taarifa zao kwani kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora” ameongeza.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa Wazee, wagonjwa, walemavu, wamama wajawazito na wenye watoto wadogo kujitokeza kwa wingi kuboresga taarifa zao kwani mazingira ni mazuri na wametoa kipaumbela kwa watu hao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima amesema katika zoezi hilo jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa kati ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20.
Amesema wapiga kura 4,369,531 wanatarajia kuboresha taarifa zao wakati wapiga kura 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendeleo kuwepo kwenye daftari hilo ambapo baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa Daftari litakuwa na jumla ya wapiga kura 34,746,638.
“Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikua na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/20 lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura”, amesema Kailima.
Ameongeza kuwa Tume tayari imekamilisha maandalizi yote ikiwemo vituo vya kuandikishia wapiga kura ambapo vipo vituo 40,126 nchi nzima Tanzania bara na Zanzibar.