Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwesse (kulia), akimkabidhi mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Mzee Ramadhan Nyamka (kushoto), muda mfupi baada ya kukamilika kwa zoezi la kutia saini makubaliano ya mauziano ya nishati hiyo, katika hafla iliyofanyika leo Juni 8,2024, Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Mzee Ramadhan Nyamka (kushoto), akioneaha mkaa aliokabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse katika hafla hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwasse, akizungumza muda mfupi kabla ya zoezi la kutia saini makubaliano ya mauziano ya nishati safi ya mkaa mbadala wa kupikia (Rafiki Briquettes) na Jeshi la Magereza. Makubaliano hayo yamefanyika leo Juni 8,2024 katika Ofisi za STAMICO Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Mzee Ramadhan Nyamka (kushoto), akizungumza muda mfupi baada ya kusaini makubaliano hayo.
Na: Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Jeshi la Magereza Tanzania limeingia makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ya mauziano ya nishati safi ambayo ni mkaa mbadala wa kupikia (Rafiki Briquettes) unaozalishwa na Shirika hilo, ikiwa ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi ya kupikia,
Makubaliano hayo yamesainiwa katika hafla fupi iliyofanyika leo Juni 8,2024 katika Ofisi za STAMICO Jijini Dar es Salaam, na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Mzee Ramadhan Nyamka, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk.Venance Mwasse.
Sambamba na makubaliano hayo, pia Shirika hilo limeingia mkataba wa ushirikiano na Jeshi la magereza kwaajili ya kuendeleza utafiti na uchimbaji wa maeneo yenye leseni ya uchimbaji madini.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse, amesema kuwa kutokana na uwekezaji uliofanywa na Shirika hilo kuna uhakika mkubwa wa upatikanaji wa nishati hiyo mbadala kwa muda wote, na kwamba itawapunguzia kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuni.
“Uzalishaji utakuwepo mkubwa kwani mwisho wa mwezi huu tunakwenda kukamilisha ujenzi wa viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa.
“Kiwanda kimoja kipo Kisarawe mkoani Pwani na kingine kipo Kiwira mkoani Mbeya.
Aidha amebainisha kuwa hadi sasa katika Bandari ya Dar es Salaam tayari kuna makontena 14 yenye urefu wa futi 40 yenye mitambo ya kuzalisha mkaa huo, na kwamba itakwenda kufungwa mkoani Dodoma na Tabora.
Akizungumzia mkataba wa uchimbaji madini, Dk. Mwasse amesema STAMICO ina uzoefu wa zaidi ya miaka 50 kwenye tasnia ya madini, hivyo wanakwenda kuunda kikosi kazi katika kutekeleza makubaliano ya mkataba huo ambao ni utafiti na uchimbaji wa madini hasa ikizingatiwa Shirika hilo lina wafanyakazi wa kutosha wenye uzoefu katika sekta hiyo.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza amesema utiaji saini baina ya taasisi hizo mbili ni muendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia aliyoyatoa tarehe 8 Mei mwaka huu wakati akizindua mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwamba taasisi zote zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku, zianze kutumia nishati safi ya kupikia.
“Leo nimekabidhiwa mkaa rafiki ambao unatokana na masalia ya madini, mkaa huu utatufanya tuondokane na matumizi ya kuni na mkaa, hivyo na sisi magereza tutakuwa tumechangia uhifadhi na utunzaji wa mazingira yetu hasa ikizingatiwa tumeambiwa kuna hifadhi ya kutosha ya mkaa huu katika kutumika kulisha magereza yote nchini kwa miaka mingi ijayo,” amesema.
Amesema jeshi hilo linayo magereza 129 yenye uwezo wa kuhifadhi wafungwa 29,902 kwa siku nchini ambapo wafungwa hao huhitaji huduma za malazi, chakula na matibabu.
Amesema chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwenye magereza ni kuni na mkaa, hivyo kwa siku magereza hayo yanatumia kuni zenye ujazo wa mita 91,591.25 kwaajili ya kupikia.
“Ukiangalia tasfiri yake ni miti mingi sana inabidi ikatwe kwa siku ili kuwezesha kuwapikia wafungwa chakula. Sasa tunakwenda kuondokana na uharibifu wa mazingira kupitia makubaliano haya,” amesema na kuongeza;
“Pia ndani ya magereza tunaenda kupata faida ya kulinda afya za wapishi ambao ni wafungwa na askari wanaosimamia kutokana na moshi uliokuwa unatokana na kuni na mkaa.
“Kwa hiyo mahitaji ya mkaa huu mbadala ni tani 1,047 kwa mwaka.
“Matumizi yake tunaamini pia yataongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake,” ameongeza.