Home LOCAL SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA MADHEHEBU YA DINI-MAJALIWA

SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA MADHEHEBU YA DINI-MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa kwa kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kuimarika bila ushirikiano na ushirikishwaji wa kila mtu.

Amesema hayo leo (Jumapili Mei 26, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya kuwekwa wakfu kwa askofu msaidizi wa jimbo kuu katoliki Mbeya Mshashamu Godfrey Jackson Mwasekaga na Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji jimbo kuu la Mbeya, iliyofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Cardinali Pengo.

“Ni ukweli usiopingika uwepo wa Taasisi za Dini unasaidia katika kuchangia juhudi za Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kama vile elimu, afya, kilimo, maji na fedha, huduma ambazo Serikali peke yake isingeweza kuzifikisha kwa wananchi mara moja”.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalipongeza kanisa Katoliki kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za jamii kwa Watanzania.

“Hapa Mbeya na Mkoani Songwe ninafahamu kuwa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya linashirikiana na Serikali katika kutoa huduma afya katika maeneo 15 ya kutolea huduma ikiwemo Hospitali mbili za Igogwe iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na Mwambani iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Vituo vya Afya vitatu (viwili Mkoa wa Mbeya na kimoja Mkoa wa Songwe); Zahanati 10 (7 zipo Mkoa wa Mbeya na 3 Mkoa wa Songwe)”

Pia, amewakikishia viongozi wa dini kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na madhehebu yote ya dini pamoja na wadau wote katika kuhakikisha huduma bora za afya na elimu hapa nchini zinapatikana

Kadhalika Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa dini waendelee kuweka msisitizo katika masuala ya kuwekeza katika vijana na kukemea vitendo vyote hatarishi kwa vijana mfano matumizi ya dawa za kulevya, wizi, ubakaji na kadhalika.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya viongozi wa madhehebu ya dini ya kuwaongoza watu kiroho kwa kuwapa mafundisho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema kuwa Kanisa linatambua mchango mkubwa wa Serikali na kuunga mkono mipango ya maendeleo katika utoaji huduma za maji, umeme, barabara, afya na maeneo mengine.

“Kanisa linatoa pongezi kwa Serikali kwa utekelezaji wa programu mbalimbali za kumpunguzia mwananchi changamoto za kiuchumi na jamii”.

Kadhalika Askofu Mkuu Nyaisonga ameipongeza Serikali kwa kupinga vitendo vya ushoga na usagaji “endeleeni msimamo huo, kanisa lina msimamo imara wa kupinga vitendo hivyo”.

Previous articleTANZANIA YASAINI MKATABA WA KIHISTORIA WA KIMATAIFA WA WIPO
Next articleSOMA MAGAZETI YA LEO JUMATATU MEI 27-2024
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here