DAR ES SALAAMÂ
Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama amewataka watanzania kuendelea kuyakumbuka na kuyaenzi mambo mema aliyoyafanya hayati Benard Membe wakati wa uhai wake na kuona namna gani ya kuendelea kuyasimamia yale mema ambayo alikuwa anataka yatekelezwe.
Msama ameyasema hayo leo katika misa ya kumkumbuka Hayati Benard Membe iliyofanyika katika kanisa la St. Joseph Jijini Dar es Salaam ambapo kesho anatimiza mwaka mmoja tangu kufariki kwake.
Msama amesema Hayati Membe ameacha alama ndani ya serikali wakati akiwa waziri wa mambo ya nje, kwani matunda na alama aliyoicha inaigusa nchi.
“Sasa unatimia mwaka mmoja tangu Hayati Membe atutoke ambapo ametuachia mambo mengi, kuna mambo mengi amefanya katika Taifa letu na kuna mambo mengine ambayo ametuachia ili sisi tuyaendeleze. Kikubwa ambacho ametuachia sisi watu wake wa karibu, tuwe wamoja, tuwe tunasameheana tunapokoseana, tusiwe watu wa visasi, tusiwe watu wa kuzungumziana mambo ambayo Si sahihi, na ametuachia tuwe wazalendo katika Taifa letu la Tanzania ili tuweze kuwasaidia na wengine ambao wanatakiwa kuinuliwa”
“Tusisahau kumcha mungu, tuwe tunajitolea sana katika kazi za mungu, tuwe tunasaidia sana miradi ya kazi za mungu kuhakikisha kwamba kazi za mungu zinasonga mbele. Sisi watu wake wa karibu na Hayati Membe, tunaendelea kuyaenzi yale ambayo yanatakiwa kuyafanya”
Kwa upande wake Waziri wa Habari , Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wamekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya Hayati Membe nchini, hasa katika jimbo la mtama ambapo ndipo alipozaliwa.
“Tumeandaa Misa kwaajili ya kumkumbuka kaka yetu Benard Membe ambapo kesho tarehe 12 atakuwa anatimiza mwaka mmoja tangu afariki, tumekuwa na siku nzuri ya kutafakari kazi nyingi alizozifanya katika nchi yetu, katika jimbo la mtama ambapo ndipo alipozaliwa”
“Kuna mambo aliyaanzisha na hapa ndiyo ilikuwa tafakari kubwa, kuna mambo aliyaanzisha kwa kanisa ambalo alikuwa akihudumiwa ikiwemo baadhi ya ujenzi wa makanisa na majengo mbalimbali ya kanisa, ambapo tumekubaliana tuangalie namna ambayo tutazikamilisha Zile ndoto alizozianzisha”
Waziri Nape amesema kwa upande wa Mtama, Hayati Membe alikuwa ni muumini wa kubadilisha maisha ya watu kwani wakati wa uongozi wake alikuwa akitamani kila mtu awe na maisha mazuri.
“Alitamani mtu aishi kwenye nyumba nzuri, apate maji safi, na hizi ndizo ndoto ambazo nimeendelea nazo, ndiyo maana tangu aliponiacha tumehakikisha tumesambaza umeme Jimbo Zima, tumepeleka maji Kila Mahali, mawasiliano, shule, na katika Kijiji na Kata aliyotoka wakati anaondoka hakukuwa na sekondari, hivyo tumejenga sekondari na tukaipa jina lake Benard Membe ili kumkumbuka kuwa alikuwa ni mtu ambaye alipenda kubadilisha maisha ya watu anaowaongoza”
Naye Mke wa Hayati Benard Membe, Dorcas Membe aliwashukuru watu wote walioshirikiana nao kwenye maandalizi ya misa hiyo, hivyo ameomba upendo, ushirikiano uendelee kuwepo kati ya ndugu, jamaa na marafiki