KIGOMA
Kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa asilimia 97 ya mashauri yaliyowasilishwa kwenye Baraza la Ushindani nchini (FCT) kumechochea na kuongeza uwajibikaji kwa mamlaka za udhibiti wa huduma na biashara nchini katika kusimamia ushindani wa haki.
Hayo yamesemwa Aprili, 19, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Abbas Rugwa wakati akifungua semina ya siku moja ya utoaji wa elimu kwa wadau kuhusu shughuli za Baraza hilo.
Amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha inaweka mazingira rafiki na wezeshi ya ushindani wa haki katika biashara na utoaji huduma na kuzitaka mamlaka za udhibiti kutekeleza azma hiyo ya serikali.
“Ni lazima mamlaka za udhibiti wa huduma zihakikishe zinasimamia sheria za ushindani wa haki ili usimamizi huu ubainishe uwepo wa mazingira rafiki na wezeshi ya ushindani bila kuwepo kwa mizengwe au upendeleo kwa baadhi ya watu au taasisi nyingine,” Amesema Rugwa.
Akizungumza kwenye semina hiyo Mkuu wa Idara ya Uchumi wa FCT, Bw. Kulwa Magoti amesema lengo la semina hiyo ni kutoa elimu kwa wadau wa Mkoa wa Kigoma kuhusu shughuli za Baraza hilo na namna wadau hao wanavyoweza kulitumia kupeleka malalamiko yao ya rufaa.
Amesema tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo mwaka 2007 hadi sasa jumla ya mashauri 442 yamewasilishwa mbele ya Baraza hilo ambapo kati yake mashauri 429 sawa na asilimia 97 yamesikilizwa na kutolewa maamuzi.
Pia amesema maamuzi hayo yameongeza umakini, ubunifu, ushindani na uwajibikaji kwa wadau na mamlaka za usimamizi wa utoaji huduma na biashara nchini.
“Mamlaka zinazohusika na malalamiko na maamuzi yanayowasilishwa kwenye Baraza hili ni pamoja na Mamlaka ya udhibiti wa sekta ya maji (EWURA), Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa anga (TCCA), Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA), Mamlaka ya udhibiti wa huduma za mawasiliano (TCRA) na Mamlaka ya udhibiti wa mkondo wa juu wa Petroli (PURA),” amesema Magoti.
Wakizungumza kwenye semina hiyo wadau mbalimbali wa mjini Kigoma wamesema semina hiyo imewafungua macho kwa kiasi kikubwa kuona namna ambavyo watapigania haki zao kulingana na huduma wanazopata kutoka kwenye mamlaka za udhibiti zilizotajwa.
Mmoja wa washiriki hao Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake (TWCC) Mkoa Kigoma, Chichi Kamandwa amesema alikuwa anajua uwepo wa Tume ya ushindani (FCC) lakini hakujua uwepo wa Baraza la Ushindani (FCT) ambalo ndicho chombo cha rufaa kwa maamuzi yanayotolewa na FCC, EWURA, PURA,TCRA na LATRA
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Mkoa wa Kigoma, Bw. Kashindi Maulid amesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na tija kubwa kwao kama watu wanaopata huduma kutoka mamlaka mbalimbali hivyo imewasaidia kusimamia haki zao mahali popote watakapokuwa wakiamini kipo chombo kinachosimamia haki zao.
Mwisho.