Home BUSINESS JUHUDI ZA Dkt. SAMIA KUKUZA UTALII ZAONGEZA IDADI YA WAGENI NGORONGORO

JUHUDI ZA Dkt. SAMIA KUKUZA UTALII ZAONGEZA IDADI YA WAGENI NGORONGORO

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongo (NCAA), Richard Kiiza, akitoa mada katika kikao kazi na Wahariri wa Habari kilichofanyika leo Februari 26,2024 Jijini Dar es Salaam, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Thobias Makoba, akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi katika kikao hicho kilichoratibiwa na Ofisi hiyo Jijini Dar es Salaam.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM 

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongo (NCAA), Richard Kiiza, amesema kuwa juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kufufua sekta ya utalii mara baada ya UVIKO 19 kupitia filamu ya ‘Tanzania the Royal Tour’ zimechangia ongezeko kubwa la idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi hiyo, hadi kufikia wageni 752,232 kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.

Amsema kuwa ongezeko hilo la idadi ya wageni limekuwa na matokeo chanya, na kwamba mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka shilingi bilioni  31 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 171 mwaka 2022/2023.

Kamishna Kiiza amebainisha hayo alipokuwa akitoa mada kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kikao kazi na Wahariri wa Habari kilichofanyika leo Februari 26,2024 Jijini Dar es Salaam, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

(Picha za baadhi ya Wahariri na wadau, katika mkutano huo.)

“Idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi inatarajiwa kuendelea kuongezeka zaidi na kufikia takribani wageni 1,000,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, hususani katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2023/2024, Hifadhi imepokea wageni 534,065, idadi hii imeongezeka kwa asilimia kumi ikilinganishwa na idadi ya wageni waliotembelea Hifadhi katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023.” amesema Kamishna Kiiza.

Aidha, ameongeza kuwa mapato yanategemewa kuongezeka zaidi na kufikia takribani shilingi bilioni  200  kwa mwaka, kwani katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2023/2024 jumla ya kiasi cha  shilingi bilioni  123  tayari zimekusanywa sawa na asilimia 13, ikilinganisha na mapato yaliyokusanywa katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2022/23.

Katika hatua nyingine, Kamishna Kiiza amezungumzia zoezi la kuhamisha kwa hiari wananchi wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro, na kwamba hadi kufikia Februari 25.2024, jumla ya kaya ambazo zimeshahama kwa hiari kutoka ndani ya eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ni kaya 1042 zenye watu 6,461 na mifugo ipatayo 29,919.

Aidha Mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha doria katika kuhakikisha inakabiliana na migogoro ya mipaka, pamoja na kuzuia uvamizi wa maeneo ya Hifadhi.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jane Mihanji ameushukuru uongozi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa kikao kazi hicho ,na kusema Jukwaa hilo litaendelea kuunga mkono na kuwa mstari wa mbele katika mambo yenye maslahi mapana ya Taifa.

Previous articleTRENI YA UMEME YAFANYA MAJARIBIO KUTOKA DAR-ES-SALAAM MPAKA MOROGORO 
Next articleULINZI WA MILIKI UBUNIFU KATIKA RASILIMALI ZA KIJENETIKI NA UJUZI WA JADI KUNUFAISHA NCHI NA JAMII ZA KIJADI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here