*Atoa agizo Ofisi za CCM mikoani kuwafuatilia wote*
> _Akemea vikali tabia za kuanzisha ligi za Mbuzi Cup, Ng’ombe Cup kwa lengo la kusaka uongozi huo kabla ya muda_ .
> _Asema Wanaojaribu kutaka Ubunge kwa sasa Chama kitawaweka pembeni wote ifikapo 2025_
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Ndugu Anamringi Macha ametoa onyo kwa wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, kuacha kuvunja kanuni, vinginevyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Amewataka wanachama wote wenye nia ya kuwania uteuzi wa kugombea nafasi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi kupitia CCM, kusubiria wakati sahihi ambao utatangazwa kwa mujibu wa taratibu za Kikatiba, Kanuni, Miongozo na maelekezo mbalimbali ya Chama.
Ndugu Anamringi ameyasema hayo Jumapili Desemba 31, 2023, wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Jimbo la Ubungo, ambapo Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo (CCM), alisoma na kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, kwa mwaka 2023, kwenye Ukumbi wa Mrina Hall, jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Macha pia amewataka wanachama wa chama hicho kuwapa ushirikiano viongozi walioko madarakani ili waendelee kutimiza majukumu yao kwa ufanisi bila bugudha.
“Miaka bado haijaisha maana kuna watu wanafikiri imeshaisha na hata kama tunaelekea sasa kwenye uchaguzi lakini muda wa uchaguzi bado haujafika, miaka iliyoisha ni mitatu ambayo ni kama 65% za muda wa kiongozi madarakani bado miwili 2024-25.”
“Si sahihi wakatokea watu kuanza kufanya kampeni za chinichini kwa sasa, niwaambie muda huo bado, muda wa kufikiria ubunge kwa jimbo bado, kufikiria udiwani na wakati madiwani wapo na bado muda wao wa kazi upo…badooo, huu bado ni muda wa wale waliopo madarakani hivyo tuwaache waendelee kufanya kazi zao kikamlifu katika kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM 2020/25,” amesema Ndugu Macha na kuongeza;
“Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi mikoa yote ya kwamba fuatilieni sana juu ya wale wote ambao wanapitapita huko kutafuta udiwani nje ya utaratibu ili siku ikifika tuwaambie kwa kwaheri kwa sababu moja ya tatizo kubwa ni kutoweka kumbukumbu hivyo tuwaite na tuwaambie kuwa wanachofanya sio sahihi.”
Amesema kuwa CCM Makao Makuu inawafuatilia kwa karibu wanachama wote
‘wanaojipitisha pitisha’ wakitaka kuwania ubunge kinyume cha taratibu.
“Tutawaeleza Wanachama wetu nchi nzima ya kwamba wale wote ambao wanajaribu kuanza kuvunja taratibu za kutafuta uongozi, wao waendelee ila mwezi wa 9 mwaka 2025 watakuja kujuta tutawaweka pembeni. Unakuta mbunge yupo bungeni halafu unasikia huko Ubungo kumeanzishwa mbuzi cup. Achaneni na hizo ligi za uongo kama kweli unasaidia Chama, fika kwa Katibu wa Chama aongee na Mwenyekiti waone na waseme huyu ni mpenzi wa Chama Cha Mapinduzi anatoa hiki kusaidia au kuchangia na sio kukimbizana usiku usiku,” ameongeza Ndugu Macha.
Mbali ya kupokea taarifa hiyo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kutoka kwa mbunge, Ndugu Macha pia alikabidhi pikipiki nane kwa ajili ya Ofisi za CCM kwenye kata zote nane za jimbo hilo ili kurahisisha shughuli mbalimbali za utendaji, zikiwa zimetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
#CCMImara
#KaziIendelee
#TunaendaNaSamia
#VitendoVinaSauti